Shomari Kapombe Simba SC
Simba SC

Kapombe Arudisha Matumaini Simba SC Ligi ya Mabingwa Afrika

Vardo October 29, 2026 9:33 am

BEKI uzoefu wa Simba SC, Shomari Kapombe, ameweka wazi kuwa uzoefu wa kukutana na wapinzani wao wa zamani katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) utakuwa silaha kuu ya kuwavusha na kufanya vizuri msimu hii.

Simba SC imepangwa katika Kundi C lenye ushindani mkubwa ikijumuisha miamba RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates kutoka Afrika Kusini, pamoja na Colombe Sportive ya Cameroon.

Akizungumzia ratiba na kundi hilo, Kapombe alisema kuwa uwepo wa timu ambazo wameshacheza nazo huko nyuma unalipa benchi la ufundi urahisi wa kuandaa mbinu sahihi za ushindi.

“Kwanza tunashukuru Mungu kwa kuona kundi letu na kuwafahamu wapinzani wetu. Jambo la kutoa matumaini ni kwamba katika kundi hili, kuna timu moja tu tutakayokutana nayo kwa mara ya kwanza. Hizo mbili nyingine tayari tunazijua vizuri na tuna uzoefu nazo,” alisema Kapombe.

Beki huyo wa kulia ana kumbukumbu nzuri dhidi ya Orlando Pirates katika msimu wa 2021/22 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo alifanikiwa kufunga bao muhimu katika mchezo wa nyumbani uliopigwa jijini Dar es Salaam.

Kapombe ameongeza kuwa kikao cha wachezaji na benchi la ufundi kipo tayari kwa ajili ya maandalizi ya kina ili kuhakikisha wanaanza kwa kasi na kutinga hatua ya robo fainali.

“Tuna imani kubwa na maandalizi yetu. Lengo letu ni kuhakikisha tunafanya maandalizi bora zaidi ili tuwe tayari kwa ushindani wowote uliopo mbele yetu,” alisisitiza.

Msimu huu, Simba SC inalenga kwenda mbali zaidi katika michuano hiyo ya kimataifa, huku ikitegemea zaidi wachezaji wake waandamizi kama Kapombe kutoa mwongozo na hamasa kwa kikosi kizima.

Magori Atoa Onyo Kundi C: “Uhuru Kusiwe na Uhuru”, Simba Yapania Pointi 9 Nyumbani CAF Champions League Steve Barker: Simba SC Inaweza Kutwaa Ubingwa Afrika, Lakini…