Clement Mzize Aivusha Yanga SC: Aeleza Siri ya Bao la Ushindi Dhidi ya Mashujaa FC
MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Clement Mzize, ameweka wazi kuwa bao la ushindi alilofunga dhidi ya Mashujaa FC limempa morali na hamasa kubwa ya kuendelea kuonyesha kiwango bora zaidi msimu huu, baada ya kurejea uwanjani akitokea kwenye majeraha ya muda mrefu.
Mzize aliingia kipindi cha pili katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati matokeo yakiwa sare ya 1-1, kabla ya kuifungia Yanga bao la pili na kupambania ushindi wa mabao 2-1 ugenini.
Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Mzize msimu huu tangu arejee uwanjani, huku kiwango chake bora kikimwezesha kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mchezo (Man of the Match).
Akizungumzia kurejea kwake kwa kishindo, Mzize alieleza kuwa matokeo hayo ni zao la kazi kubwa aliyoifanya mazoezini kipindi chote alichokuwa akiuguza majeraha.
“Nashukuru Mungu kwa kurejea salama. Bao langu la kwanza msimu huu limenipa morali kubwa kwa sababu nimekuwa nikilifanyia kazi sana mazoezini. Ninaamini nitaendelea kufanya vizuri kila nitakapopata nafasi ya kucheza,” alisema Mzize.
Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa hakuwahi kupoteza imani ya kurejea katika kiwango chake cha juu, na lengo lake kuu lilikuwa ni kutumia vyema kila nafasi atakayopata ili kuisaidia Yanga kuondoka na pointi tatu muhimu.
Kando na jitihada zake uwanjani, Mzize hakusita kuwashukuru mashabiki wa Wananchi kwa ushirikiano na sapoti kubwa waliyompa wakati akiwa nje ya uwanja.
“Sapoti ya mashabiki imekuwa chachu kubwa ya kunipa moyo wakati wa kipindi kigumu cha kujiuguza. Naendelea kujipanga ili kuimarisha kiwango changu zaidi na kuisaidia timu kwenye michezo inayofuata,” alihitimisha Mzize.
Kurejea kwa Mzize na kuanza kufunga ni habari njema kwa benchi la fundi la Yanga SC na mashabiki wake, kwani kunaongeza nguvu na ufanisi kwenye safu ya ushambuliaji katika mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.