Magori Atoa Onyo Kundi C: “Uhuru Kusiwe na Uhuru”, Simba Yapania Pointi 9 Nyumbani CAF Champions League
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, amewataka mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru kwenye michezo ya nyumbani ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, akesisitiza kuwa hakuna timu itakayopata nafasi ya kucheza kwa amani mbele ya Wanasimba.
Magori ameeleza kuwa malengo makuu ya Simba SC ni kushinda mechi zote za nyumbani ili kukusanya pointi tisa (9), kisha kupambana kupata pointi muhimu ugenini ili kutimiza azma ya klabu hiyo kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Simba SC imepangwa katika Kundi C ikijumuisha miamba ya soka barani Afrika: RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, na Colombe Sportive ya Cameroon. Magori amekiri kuwa kundi hilo lina ushindani mkubwa unaohitaji maandalizi ya dhati na umakini wa hali ya juu.
“Ni kundi gumu, hakuna timu rahisi katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Lazima tupambane na kushinda mechi zote za nyumbani, kisha tutafute ushindi au sare mbili ugenini,” amesema Magori.
Uchambuzi wa Wapinzani wa Simba SC Kundi C
Akiwachambua wapinzani wa Wekundu wa Msimbazi, Magori amebainisha uzoefu na ubora wa kila timu:
-
RS Berkane (Morocco): Mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika, wakiwa na historia ya ushindani mkubwa na Simba SC katika miaka ya hivi karibuni.
-
Orlando Pirates (Afrika Kusini): Waamba wa soka la Afrika Kusini waliowahi kutwaa ubingwa wa Afrika na kucheza fainali za bara hili, ambapo michezo yao na Simba daima imekuwa na ushindani mkali.
-
Colombe Sportive (Cameroon): Timu asiyopaswa kudharauliwa hata kidogo kutokana na ubora na uzoefu wa soka la Afrika Magharibi.
Magori ameonya dhidi ya tabia ya mashabiki au wadau wa soka kuzichukulia baadhi ya timu kama “dhaifu” kwa kutazama majina pekee, akieleza kuwa viwango vya soka la Afrika vimepiga hatua kubwa.
“Watu wamezoea majina, lakini mpira wa sasa duniani si majina tena—ni uwanjani na uwezo wa wachezaji. Kama timu imekuwa bingwa au imefuzu kutoka nchi kama Misri, Morocco au Algeria, hiyo si timu rahisi hata kidogo,” alisisitiza.
Wito kwa Wanasimba: “Uwanja wa Uhuru Kusiwe na Uhuru”
Katika kuhakikisha Msimbazi inatumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani, Magori ametoa rai kwa mashabiki kuugeuza Uwanja wa Uhuru kuwa ngome asiyoingilika mpinzani wowote.
“Kwa mashabiki tujiandae, tuhakikishe pointi tatu muhimu zinapatikana pale Uhuru. Uhuru kusiwe na uhuru tena; kila timu ikija iupate moto kwa sababu hakuna amani pale. Tukiwa na pointi tisa nyumbani na kuchukua pointi chache ugenini, safari yetu ya robo fainali itakuwa wazi,” alihitimisha Magori.