Lengo Letu Ni Robo Fainali! Steve Barker Atuma Onyo Kali Ligi ya Mabingwa
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amewasha moto mapema kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akisisitiza kuwa kikosi chake kimejipanga kufanya makubwa na hakina nafasi ya kuwaza kushindwa licha ya kupangwa kwenye kundi lenye ushindani mkubwa.
Simba imejumuishwa katika Kundi C lenye vigogo wengine kama RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, na Colombe Sportive ya Cameroon kwenye droo iliyosheheni timu zenye uzoefu mkubwa barani Afrika.
Akizungumzia kundi hilo, Barker amekiri kuwa ni gumu lakini akaweka wazi kuwa anamfahamu vizuri RS Berkane kutokana na historia yao ya kukutana huko nyuma wakati akiwa kocha wa Stellenbosch ya Afrika Kusini, huku akiitaja Orlando Pirates kuwa ni timu bora inayoiwakilisha vyema soka la Afrika Kusini.
“Ni kundi lenye changamoto na timu bora, lakini hatuogopi mtu. Ninaifahamu vizuri RS Berkane na hata Orlando Pirates. Lengo letu ni kuanza kwa nguvu na kusonga mbele,” alisema Barker.
🔴 RS Berkane ni Tishio, Lakini Hatuogopi!
Kocha huyo alionya kuwa klabu ya RS Berkane inapaswa kupewa heshima kubwa kutokana na ubora wao wa mara kwa mara katika michuano ya CAF misimu ya hivi karibuni. Hata hivyo, alisisitiza kuwa nguvu za Simba zitaelekezwa kwenye maandalizi na sio kuwatazama wapinzani kwa hofu.
🔥 “Hatufikirii Kushindwa!”
Barker alihitimisha kwa kutoa kauli nzito iliyowapa matumaini makubwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi, akieleza kuwa neno “kushindwa” halipo kwenye kamusi yao ya msimu huu:
“Lengo letu kuu ni kufuzu hatua ya mtoano. Hatufikirii kabisa kushindwa; tutafuzu, hiyo ndiyo shabaha yetu kwa asilimia mia moja. Hatutaki hata kuwa na maneno ya kutofuzu kwenye msamiati wetu.”