Simba SC Kuituliza RS Berkane na Orlando Pirates Ligi ya Mabingwa Afrika: Ahmed Ally Afunguka
Klabu ya Simba SC imeweka wazi dhamira yake ya kulipa kisasi dhidi ya RS Berkane ya Morocco na Orlando Pirates ya Afrika Kusini baada ya timu hizo kupangwa pamoja katika Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Uongozi wa Wekundu wa Msimbazi umesisitiza kuwa safari ya msimu huu haina malengo mengine zaidi ya kufika hatua ya nusu fainali na hatimaye kupambana kuwania ubingwa wa bara la Afrika.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameeleza kuwa kikosi chao kipo katika kiwango bora na kimejipanga kurekebisha makosa ya misimu iliyopita ili kuandika historia mpya katika soka la kimataifa.
Ahmed Ally: “Hili ni Kundi la Kuongoza na Kuwa Kinara”
Katika droo ya hatua ya makundi, Simba SC imepangwa Kundi C ikijumuisha miamba hiyo miwili pamoja na Colombe Sportive kutoka Cameroon. Ahmed Ally amebainisha kuwa kundi hilo ni jepesi kwa Simba iwapo wachezaji watatekeleza wajibu wao kwa asilimia 100.
“Tumepangwa kundi ambalo lina RS Berkane na Orlando Pirates. Ni kundi jepesi kama tutatimiza wajibu wetu kwa asilimia 100. Tukifanya hivyo, hili ni kundi la kuongoza na kuwa kinara,” alisema Ahmed Ally.
Msemaji huyo aliongeza kuwa Simba inazifahamu vyema RS Berkane na Orlando Pirates kutokana na historia ya mechi zao za nyuma, tofauti na Colombe Sportive ambayo wanaendelea kuifuatilia kwa karibu.
Hesabu za Kisasi: RS Berkane na Orlando Pirates
1. RS Berkane (Morocco)
Akizungumzia miamba ya Morocco, Ahmed Ally alisema Simba ina deni kubwa la kulipa baada ya kupoteza dhidi yao katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, matokeo ambayo anaamini yalitawaliwa na mazingira magumu nje ya uwanja.
“RS Berkane alitunyang’anya ubingwa msimu uliopita kwenye Kombe la Shirikisho. Tunaamini hakutunyang’anya ubingwa kwa sababu ya ubora wake tu, bali kulikuwa na fitna na fiksi nyingi. Sasa tumekutana tena Ligi ya Mabingwa Afrika; tutakutana nyumbani kwao na hapa Tanzania. Tutawaonyesha Simba ni watu wa aina gani,” alisisitiza.
2. Orlando Pirates (Afrika Kusini)
Kuhusu Orlando Pirates, Simba inakumbuka kuondolewa kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2021/22 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.
“Msimu uliopita tulishindwa kwenda nusu fainali kwa sababu ya Orlando Pirates. Tulipata bao moja Benjamin Mkapa, nao wakapata bao moja kwao, kisha wakatutoa kwa penalti. Sasa muda wa kulipizana umefika. Mwaka huu tunakwenda kuwanyima usingizi na amani,” alisema.
Maandalizi na Mshikamano Ndiyo Chachu ya Mafanikio
Licha ya kujiamini, Ahmed Ally alitaka timu isidharau Colombe Sportive ya Cameroon. Alibainisha kuwa nidhamu ya mchezo na maandalizi thabiti kuanzia miezi ya Desemba, Januari hadi Februari zitakuwa nguzo kuu za kufuzu.
Alimalizia kwa kuwataka mashabiki wa Simba SC kuendelea kuungana na kuipa timu support katika mechi zote za nyumbani na ugenini ili kutimiza lengo la kufika nusu fainali na kutwaa ndoo ya Afrika.