Clara Luvanga Washington Spirit
Michezo Bongo

Clara Luvanga Aipeleka Washington Spirit Fainali NWSL kwa Bao la Ushindi!

Vardo November 15, 2026 11:21 am

WASHINGTON, MAREKANI – Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga, ameendelea kuandika historia nchini Marekani baada ya kufunga bao la ushindi lililoipa Washington Spirit ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Utah Royals na kukata tiketi ya kucheza fainali ya Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL).

Katika mchezo huo wa nusu fainali uliopigwa Jumamosi Novemba 14, 2026 kwenye Uwanja wa Audi Field, Washington DC, Luvanga aliibuka shujaa dakika ya 56 baada ya kunasa pasi fupi ya kurudi nyuma iliyopigwa kimakosa na beki wa Utah Royals, Nuria Rábano, na kuukwamisha mpira wavuni.

Bao hilo linamfanya nyota huyo aliyejiunga na klabu hiyo Septemba mwaka huu kufikisha mabao manne na pasi za mabao (assists) tatu katika mechi saba alizocheza, akiwa amehusika moja kwa moja kwenye mabao saba hadi sasa.

Mchezo Ulivyokuwa

Wageni Utah Royals ndio walikuwa wa kwanza kuwashtua wenyeji kwa kupata bao la kuongoza dakika ya pili kupitia kwa Cloé Lacasse. Lacasse alifunga bao hilo kwa mpira wa kona ulioenda moja kwa moja wavuni ndani ya dakika moja na sekunde 57, likiweka rekodi ya kuwa bao la haraka zaidi katika historia ya hatua ya mtoano ya NWSL.

Hata hivyo, Washington Spirit haikukata tamaa na ilisawazisha dakika ya nane kupitia kwa Sofia Cantore aliyemalizia pasi safi ya nyota Trinity Rodman, matokeo yaliyodumu hadi mapumziko kabla ya Luvanga kuhitimisha ushindi kipindi cha pili.

Rekodi ya Kihistoria na Fainali

Ushindi huo unaifanya Washington Spirit kutinga fainali ya NWSL kwa mara ya tatu mfululizo, ikiwa ni klabu ya pili kufikia mafanikio hayo baada ya North Carolina Courage kufanya hivyo kati ya mwaka 2017 na 2019.

Fainali hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Audi Field Novemba 21, 2026, ambapo kwa mara ya kwanza Spirit watacheza mchezo wa kuwania ubingwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani. Sasa wanasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Gotham FC na Kansas City Current.

Zimamoto FC Yatangaza Vita ya Ubingwa 2026-2027, Ibrahim Ramadhan Afichua Siri ya Bares! Charles Masai: Kiungo na Meneja wa KenGold Anayezigomea Simba na Yanga