Uchaguzi Mkuu wa Simba: Julio, Mkwabi na Sasali Wachukua Fomu TFF
Pazia la zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu ya Simba SC limefungwa rasmi leo katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), huku matukio ya kusisimua na majina mazito yakizua gumzo kubwa miongoni mwa wanachama.
Tangu dirisha hilo lilipofunguliwa Jumatatu iliyopita, joto la uchaguzi limekuwa likipanda taratibu, lakini leo ilikuwa siku ya hukumu ambapo hadi kufikia saa 10:30 jioni, ofisi za TFF ziligeuka kuwa kivutio cha aina yake kutokana na hekaheka za wagombea waliokuwa wakipishana milangoni kukamilisha taratibu za mwisho.
Julio Amchomekea Mangungu Mchana Kweupe Kivutio kikubwa zaidi leo kimekuwa ni mkongwe na mchezaji wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye ameonyesha kuwa bado ana chenga za maudhi nje ya uwanja. Awali, Julio alirejesha fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, lakini kabla wino haujakauka, akachukua fomu nyingine nzito ya kuwania kiti cha Mwenyekiti wa klabu hiyo!
Akizungumza kwa kujiamini, Julio amefichua siri ya uamuzi huo wa ghafla akisema alimsubiri Mwenyekiti wa sasa, Murtaza Mangungu, hadi saa nane mchana bila kumuona akitokea kuchukua fomu.
“Nimeamua kuingia mwenyewe baada ya kuona kimya. Nina historia kubwa na klabu hii na ninaamini nina uwezo tosha wa kuiongoza Simba,” alitamba Julio.
Mkwabi Aibuka na Mkwara wa Mechi ya JKT Baada ya Soka la Bongo kuripoti juzi kuwa Swedi Mkwabi alikuwa amechukua fomu kwa njia ya mtandao, leo kigogo huyo alijitokeza hadharani katika ofisi za TFF kuirejesha rasmi fomu yake ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti.
Hata hivyo, Mkwabi hakuwa na maneno mengi ya kisiasa kwani alionekana kuwa na haraka ya kuelekea kwenye majukumu mengine mazito, akieleza kuwa anawahi kufanya maandalizi ya mchezo wa Simba dhidi ya JKT uliopangwa kupigwa leo.
Sam Sasali Ataka ‘Damu Mpya’ Msimbazi Kinyang’anyiro cha uenyekiti kimezidi kunoga baada ya mwanachama wa Simba SC na mwandishi wa habari maarufu, Sam Sasali, naye kujitosa rasmi kwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya juu.
Sasali amesema ameamua kuingia ulingoni ili kuleta fikra mpya na mabadiliko yenye tija, akisisitiza kuwa wakati umefika wa klabu hiyo kupata “damu mpya” yenye mitazamo tofauti kukabiliana na changamoto za soka la kisasa, ingawa hakusita kuwapongeza viongozi waliopo kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Yenga Naye Ajitosa Kwenye Ujumbe Katika hatua nyingine, mwanachama mwingine wa klabu hiyo, Yusuph Omar Yenga, alifika ofisini hapo majira ya mchana na kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe, akiahidi kuwa lengo lake kuu ni kuchangia mawazo ya kimaendeleo na kusukuma mbele gurudumu la mabadiliko ndani ya Msimbazi.
Kwa sasa, macho na masikio ya Wanasimba wote yanaelekezwa kwenye hatua inayofuata ya mchujo na usaili ili kuwajua wale watakaopenya kwenye kinyang’anyiro hicho cha kihistoria.