NA SALEH ALLY
MJADALA umekuwa mkubwa sana kuhusiana na viungo wawili, mmoja ni Ibrahim Ajibu ambaye ameichezea Yanga msimu uliopita na Jonas Mkude wa Simba.
Hawa wote ni vijana wa Kitanzania ambao tayari wamejitengenezea ajira kupitia mchezo wa mpira wa miguu.
Ni jambo guri sana kumuunga mkono mwenzako unapoona amefanikiwa katika jambo fulani. Sisi sote ni Watanzania, lazima tuungane mkono kwa maana ya kila mmoja anapaswa kuishi kwa furaha.
Pamoja na kuungana mkono, kunapofikia wakati kuna ukweli unapaswa kuwa wazi, unapaswa kuwa na njia iliyonyooka kwa ajili ya kulisaidia taifa letu basi ni vizuri kuwa hivyo.
Kwa sasa tuna msala wa Ajibu na Mkude kwa sababu ya mapenzi ya klabu kubwa mbili za Yanga na Simba. Bahati mbaya nimeona baadhi ya mashabiki wanajaribu kuuhamisha mjadala hadi kwenda kwa Shomari Kapombe kwa kisingizio kuwa Kocha Emmanuel Amunike hawapendi wachezaji wa Simba.
Wakati mwingine inakuwa vizuri kutafakari mambo kabla ya kuanza kuyatoa. Kapombe sote tunajua ni majeruhi, Amunike alimuita huenda aliamini angeweza kupona. Anayesema kuwa Kapombe anaonewa, atuthibitishie kwamba yuko fiti ila kaachwa tu. Vizuri tuzungumze mambo ya msingi na hasa katika hili la taifa letu.
Kapombe si beki pekee, timu ya taifa haichagui watu sababu ya ushabiki wa klabu au kulazimisha. Wakati mwingine lazima tujiondoe katika ushabiki hasa kama kuna uhalisia linapofikia suala la timu ya taifa.
Acha nirejee katika suala la Ajibu na Mkude, ambao kuachwa kwao na Amunike linaendelea kufanya tusahau mjadala wa timu yetu ya taifa inafanyaje na badala yake ishu ni Ajibu na Mkude.
Tumepata taarifa ya Mkude kuchelewa kufika kambini, mmekuwa mkisikia namna Simba wakilalamika kuhusiana na utovu wa nidhamu. Ingawa wamekuwa wakifanya makosa ya kulalama chinichini.
Chinichini ya Simba, inafanya watu wengi wasijue matatizo ya Mkude na hili linasababisha hata inapotokea akatendewa haki, wengi wanaamini ameonewa. Simba wamekuwa wakificha maradhi lakini unaona “kifo” kinamuumbua.
Huyu ni kijana Mtanzania, tumtengeneze kwa kumueleza ukweli badala ya kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.
Kuna mtu alihoji kuhusiana na Ajibu, akisema kama Ajibu tatizo ni kukaba, Messi Mbona hakabi Barcelona, au Chama mbona hakabi Simba? Ana haki ya kuhoji. Lakini timu moja haiwezi kuwa na kina Messi wawili.
Taifa Stars uwe na Samatta asikabe, uwe na Ajibu asikabe, itakuwa timu ya namna gani. Mwalimu anamuachia Samatta muda wa kupanga mashambulizi na kuhifadhi nguvu. Halafu na Ajibu naye iwe hivyo!
Ndio maana anaweza kuona bora kuwa na mchezaji asiye na kipaji sana lakini akaisaidia timu inapokuwa inashambuliwa. Badala ya kuwa na timu mkianza kushambuliwa mnabaki pungufu ya wachezaji wawili, haiwezekani na hasa ukizingatia tunakwenda kama timu isiyopewa nafasi.
Binafsi mimi si mtu ninayemkubali sana Amunike kutokana na uchezaji wa timu ulivyo. Lakini bado naweza kuheshimu matakwa yake halafu tutaona kitakatochokea Misri ingawa kama Mtanzania ninaomba yawe matokeo bora kwa kuwa Amunike ni Mnigeria na sisi tumemuajiri tu.
Lazima tukubali kuwaambia ukweli vijana wetu. Lazima tupime na kuangalia, hivi kama kweli kabisa Amunike angekuwa anajua atasaidiwa na Ajibu na Mkude atawaacha vipi wakati na yeye angependa kuweka rekodi.
Mfano, mtu kaitwa na hata kabla ya kujiunga tayari kaonyesha utovu wa nidhamu.
Tukubali wakati mwingine kuwaeleza watu wetu maneno magumu ambayo yatawabadilisha badala ya kuendelea kuwa mashabiki wao wakati tunaona wanatumbukia shimoni.
Wakati huu ni mzuri kufanya mjadala kwa wale walio na kikosi cha Afcon nchini Misri na watafanya nini na Ajibu na Mkude, tuwaache na mapumziko yao.