Home Uncategorized Wanaompinga Amunike, wamesahau sababu ya Yanga kuitwa Kandambili.

Wanaompinga Amunike, wamesahau sababu ya Yanga kuitwa Kandambili.

“…mwalimu wetu ni raia wa Nigeria, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, ameshinda vikombe vya Afcon lakini ni mchezaji wa zamani wa Barcelona na timu zingine kama Zamalek…”

“…Kwa wale ambao mnaufahamu mpira hambabaishwi, ni jina kubwa kwenye ulimwengu huu wa mpira…”

Hayo ndio maneno ya awali kabisa ya Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wa utambulisho wa kocha Emmanuel Amunike.

“…Tujiulize wenyewe, timu za Afrika si nzuri? Ni nzuri ila tunakosa vitu vichache, naamini tunapaswa kuwaandaa wachezaji wetu na kuwatengeneza kufahamu changamoto za mchezo husika, ….nipo hapa na nimekuwa Mtanzania naishi na watu na tunatakiwa kufanya kazi pamoja, bila kusahau vyombo vya habari ili tuone ni jinsi gani tunaweza lisaidia soka la Tanzania”

Maneno hayo ya Amunike huenda ndio msingi wa tabia na hurka zake katika soka. Kwa kinachoendelea sasa sio cha kukishangaa wala kujiuliza, maana yake kama ni mwandishi wa fasihi, basi Amunike ana falsafa iliyokomaa na inayoeleweka, sio ya kibwenyenye.

Kuwaacha Jonas mkude na Ibrahim Ajib sio dhambi, uzuri ametoa sababu nzuri tu na zinazoweza kumuingia kila anayeitwa mdau wa soka nchini. Sababu ya kwanza ni nidhamu mbovu huku ya pili ikiwa ni uwezo mdogo uwanjani.

Kupitia sababu hizo mbili bila shaka kila kocha na anayeujua mpira lazima atakubaliana na mwalimu. Kocha humchagua mchezaji fulani kutokana na kiwango chake uwanjani na wala sio maneno ya mitandaoni. Nidhamu ndio msingi wa ushindi kwa timu yoyote ile hivyo Amunike yuko sahihi kupitia vigezo hivi viwili.

Kumuingilia mwalimu ni kosa katika maendeleo ya soka nchini, na kwa lugha ya kihistoria naweza iita tabia hii kama ni umwinyi.

Umwinyi umeanza zamani kulitafuna soka letu, kila kiongozi ana mchezaji wake angependa na atahakikisha anapata namba hata kama mwalimu hatakuwa na mpango naye kutokana na kiwango chake na hata nidhamu, huu ndio umwinyi!.

Umwinyi ndio ulileta mgogoro mkubwa kwa vilabu vya Sunderland na Yanga miaka ya 1975, na hapo ndipo jina la Yanga kuitwa “Kandambili” lilipozaliwa. Ngoja nikurudishe miaka hiyo kidogo…

Mwaka 1976 Ndani ya klabu ya Yanga yalitokea makundi mawili ambayo yalikuwa na itikadi tofauti na zenye kukinzana. Kundi la kwanza lilikuwa likiamini kuwa, maendeleo ya Yanga yataletwa kwa kufuata tamaduni na desturi ya Yanga yaani kuendesha klabu kimazoea ndio msingi wao, na kama atajitokeza yeyote akipinga mazoea hayo basi huyo ndiye adui wa kwanza wa klabu.

Vurugu hizi hazikuanzia hapo bali zilianzia mwaka 1973, kipindi hicho Yanga ikiwa chini ya Kocha Mkongo, Tambwe Leya. Kocha huyu alikuja na falsafa zake ambazo hakutaka zibadilike, Tambwe Leya aliamini katika soka la vijana zaidi.

Yalikuwa ni maamuzi magumu kwa Tambwe Leya kuwapa nafasi wachezaji wenye umri mdogo na kuwaacha wachezaji kama Abdullahmani Juma (Nahodha),Maulid Dilunga (Mexico), Kitwana Manara, Sande Manara (Compyuta), Gibson Sembuli, Hassan Gobbos “Wa Morocco”,Leonard Chitete, Juma Bomba, Boi Iddi, na wengine ambao ndio waliokuwa Ma father wa Yanga miaka hiyo.

SOMA NA HII  SIMBA YATINGA BUNGENI LEO, SPIKA AZINDUA KADI ZA MASHABIKI

Wachezaji hawa ndio waliokuwa na majina makubwa na ndio waliokuwa taswira ya Yanga. Kitendo hicho kiliwapa kiburi kiasi cha kujiona hata wasipofanya mazoezi nafasi ya kucheza dakika 90 watapata tu, Hii ilikuwa tofauti sana kwa Tambwe Leya.

Mkongo huyo aliwaamini wachezaji vijana kipindi hicho kama akina Mohammed Yahya Tostao,Kassim Manara, Gordian Mapango, Shaban Ufunguo, Mohammed Adolph Richard, Mohammed Mkweche, Jafary Abdullaman, Rashid Idd Chama, Juma Pondamali Mensa na wengine ambao walikuwa wameshanolewa na Mromania aliyetangulia klabuni hapo aliyefahamika kwa jina la Victor Stanculescu.

Na ikumbukwe kuwa, mwaka 1974, Simba ndio timu ya kwanza kubeba kombe la Afrika Mashariki, likianzishwa kwa mara ya kwanza, mwaka uliofuata yaani mwaka 1975, Mashindano hayo yalifanyikia Zanzibar,na Simba na Yanga ziliingia fainali, Yanga alibeba ndoo baada ya kumtungua Simba goli 2-0, mwaka uliofuata yaani mwaka 1976, Mashindano hayo yalifanyikia Mombasa Kenya, Yanga walifanikiwa kuingia fainali, na awamu hii wakalala kwa goli 2-1 dhidi ya Luo Union ya Kenya.

Mwaka huohuo, mambo yaliendelea kuwa mabaya, kwani Yanga  ilitupwa nje ya mashindano ya klabu bingwa Afrika na Enugu Rangers International ya Nigeria. Katika matokeo hayo mabaya, Tambwe aliwatuhumu viongozi, meneja na baadhi ya wachezaji wakongwe kuwa ndio sababu ya matokeo hayo mabaya, viongozi nao walimlaumu Tambwe kwa kushindwa kupanga timu vizuri baada ya kutowapa nafasi zaidi ma-father wa timu “wenye Yanga yao”.

Tambwe alitishia kujiuzuru kama wachezaji kama Sunday Manara, Gibson Sembuli, Kitwana Manara na wengine wawataondolewa katika klabu hiyo, kundi la pili lilitaka kocha huyo ndio aondoke na hapo ndipo yakazaliwa makundi mawili yaani Yanga Kandambili na Yanga Raizoni.

Kundi la Yanga Kandambili ndilo lilimuunga mkono kocha Tambwe, huku Yanga Raizoni wakiwa kinyume na kocha mkuu, hawa ndio waliokuwa  Mamwinyi kipindi hicho.

Matokeo ya mgogoro huu ni kutokea kwa klabu iliyofahamika kwa jina la Pan-African Sport Club baada ya kundi la Raizoni kujitenga kutoka katika kundi la Yanga Kandambili na kuunda timu hiyo.

Muda tu ndio utakaothibitisha kama akili za wazee wa zamani wa Yanga na mashabiki wa Taifa Stars wa sasa wana ufanano wa kiakili katika mlingano sahili, yaani baadae kocha Amunike atatakiwa ajiuzulu baada ya kushindwa kufanya chochote Afcon msimu huu.

Hofu yangu ni kuigawa timu yetu ya taifa katika makundi mawili yaani Simba na Yanga. Maana yake bado kuna “umwinyi” katika soka letu na hiki kinaweza kikawa chanzo cha kushindwa kufika popote licha ya juhudi kubwa zilizofanywa katika harakati za kufuzu.

Hivyo katika uhalisia, hiki kinachoendelea sasa, kinaweza kuiharibu nia ya timu ya Taifa kufanya vizuri katika michuano ya Afcon msimu huu. Watanzania hatuna budi kuungana, ni lazima tukubali kuwa mwalimu ndiye mwenye taaluma na tuukubali uwezo wake.

Tukutane Misri.

The post Wanaompinga Amunike, wamesahau sababu ya Yanga kuitwa Kandambili. appeared first on Kandanda.