Home Uncategorized KAMA WAMEKWATA KWA MAAMUZI YA KOCHA INAPENDEZA, TUINGE MKONO TIMU YETU YA...

KAMA WAMEKWATA KWA MAAMUZI YA KOCHA INAPENDEZA, TUINGE MKONO TIMU YETU YA TAIFA


MIAKA 39 si jambo jepesi kuamini kwamba ilikatika bila Taifa letu kuwa na mwakilishi kwenye michuano ya Afcon na hatimaye ndoto ya siku nyingi  imetimia sasa ni zamu yetu kuipeperusha Bendera.

Ukizungumzia Taifa ni lazima liungane kwa ajili ya kuwapa sapoti vijana ambao wameaminiwa kupeperusha Bendera kwenye michuano ya Afcon ambayo inatarajiwa kuanza Juni 21 nchini Misri ambapo timu yetu ya Taifa imeweka kambi.

Kitu cha msingi ni watanzania kuungana na kuwaombea wachezaji wetu ambao ni wawakilishi wetu kufanya vema ili kuendeleza tabasamu ambalo tumekuwa nalo hasa baada ya kufuzu michuano hiyo mikubwa Afrika.

Kabla sijaenda mbali kwanza hebu niweke wazi suala hili ambalo limekuwa lina uchungu kidogo ingawa wenye mamlaka wenyewe hawajapenda kulizungumzia lilitokea kabla hata Stars hawajekwea pipa kuelekea Misri.

Ni kuhusu kuumia kwa mchezaji Shomari Kapombe, hapa kulitokea mkanganyiko kidogo ambao uliligawa Taifa kwa muda kwani hakuna ambaye alikuwa anaujua ukweli zaidi ya mabishano kati ya wahusika ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na mchezaji mwenyewe.

Sasa kama ni masuala ya taarifa ni lazima ziwe na uhakika na zisilete mkanganyiko kwani Taifa kwa sasa lazima liungane lisiwe na makundi ya aina mbili hii ni mbaya kwetu.

Bado tuna safari ndefu ya kutafuta mafanikio ambayo kuyapata sio kitu chepesi kama ambavyo wengi wanafikiria hivyo ni lazima kutengeneza njia ya kweli.

Kapombe naye ni binadamu pia na mtoa taarifa naye ni binadamu ni lazima awe makini wakati mwingine kuweka usawa na ukweli wa mambo.

Kuna umuhimu kwa Shirikisho licha ya kuwa na mamlaka kuomba radhi kwa uongozi wa timu pamoja na mashabiki kiujumla ili kuacha kuwagawa watu kwa makundi.

Sasa tunalifunga jumla suala la Kapombe tunageukia timu yetu ya Taifa ya Tanzania kazi ni moja kuwaunga mkono kwa hali na mali.

Tumeona suala la panga ambalo limepita kwa wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa ni jambo la kawaida kwenye mchezo.

Sasa tatizo lipo kwa mashabiki kuwa na mapenzi yao yaani wanachanganya Usimba na Uyanga kwenye vitu siriazi kama timu ya Taifa ni lazima viwekwe kando kidogo.

Pia napenda kuungana na mwalimu wa timu ya Taifa Emmanuel Amunike kwa kitendo chake cha kuwaengua baadhi ya wachezaji kwa sababu ambazo amezieleza.

Kama ni kweli wachezaji walioachwa na mwalimu wameshindwa kuonyesha nidhamu pamoja na kukidhi vigezo ambavyo mwalimu anaviamini yupo sahihi.

Mchezaji yoyote ni lazima akubalike na mwalimu mwenyewe ambaye anahitaji kumtumia hivyo kazi ya maamuzi ya nani anahitajika ipo mikononi mwake.

Watanzania inabidi tuache ushabiki na badala yake tuungane na mwalimu kumpa sapoti kwa kile anachokifanya kwani hesabu zake zinajua nini anachokifanya.

Lakini kama amefanya maamuzi akiwa na yake kichwani bila kufikiria ni namna gani watanzania wanamfuatilia ni  kosa ambalo linatakiwa litafutiwe dawa.

Kwa sababu kama kuna siri nyingine nyuma ya pazia kama kulivyokuwa na mkanganyiko wa mchezaji Kapombe atakuwa hajawatendea haki wachezaji.

Kwa kufanya hivyo ule mkanganyiko ambao umekuwa ukiendelea kwa mashabiki utamalizika na kila mmoja atajua sababu ni nidhamu.

Ulimwengu wa michezo una kanuni moja muhimu kwa mafanikio ya mchezaji yoyote ni kusimamia na kuamini kwamba nidhamu ndiyo mkombozi kwa yote.

Mchezaji mwenye nidhamu ni rahisi kufikia mafanikio kwani anafuata uti wa mgongo wa kuyafikia mafanikio ambayo yamejificha hivyo ni lazima wachezaji wetu walielewe hilo.

Muda wa kupigizana kelele kwa sasa umekwisha jambo la msingi ni kuunga mkono juhudi za mwalimu kudumisha nidhamu ndani ya kikosi.

Naona namna ambavyo taifa letu linakwenda kupeperusha Bendera kwa mafanikio makubwa hasa kwa hatua ambayo tumeifikia kwa sasa.

Ikumbukwe kuwa hatua hii tumeisubiri kwa muda mrefu na kwa kuwa tumeipata basi tuitumie vema na kwa umakini tusije juta.

Nafasi ya kipekee kwa wachezaji ambao wamepata nafasi ya kujiunga na timu ya Taifa na kuonyesha uwezo wao ni lazima wapambane kiukweli kuonyesha kwamba wanaweza.

Hakuna matokeo mabaya kama kupoteza michezo yote ilihali maandalizi yamekuwa kwenye wakati sahihi na  tulitambua mapema kwamba lazima tushiriki michuano hii.

Taifa lipo nyuma yenu wachezaji linafuatilia kwa ukaribu kututoa kimasomaso hiyo Juni 21 jiandaeni vema huku mashabiki watanzania tukiendelea kuwaombea.


SOMA NA HII  WIMBO MPYA WA YANGA HUU HAPA - VIDEO