Home Uncategorized YANGA YAONYESHA JEURI YA FEDHA, USAJILI WAKE KUFURU

YANGA YAONYESHA JEURI YA FEDHA, USAJILI WAKE KUFURU


YANGA wametumia zaidi ya Sh900mil mpaka lengo likiwa ni moja tu kusuka kikosi chenye muonekano mpya na hadhi ya klabu hiyo. Fungu hilo ambalo limetokana na michango mbalimbali ya wadau na wanachama wa Yanga ni kwa kuanzia tu kwani bado mchakato unaendelea na huenda ukamalizika wiki ijayo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga ni kwamba wameweka makadirio ya Sh1.3Bil kwenye usajili na gharama nyingine za wachezaji lakini mpaka sasa wanakaribia kuvuka Sh900mil.


“Hizo fedha zimetumika kwenye gharama za tiketi na usajili wa wachezaji wapya pamoja na kulipa madeni na malimbikizo ya wale wachezaji wa zamani ambao tunabaki nao pamoja na tunaowaacha. 

“Na bado hatujamaliza, wiki ijayo ndiyo tutakamilisha mambo yote ndiyo tutakuwa na mchanganuo mzuri, ila inaweza kuzidi ile Sh1.3 Bilioni kwa vile tunataka kitu kizuri,” alidokeza kiongozi
mmoja mwenye ushawishi ndani ya Yanga.

ROSTAM AINGILIA

Bilionea mwenye mapenzi na Yanga, Rostam Azaz ameweka wazi kwamba yupo tayari kufanya lolote kwenye usajili wa Yanga kama viongozi wakihitaji msaada wake. Mfanyabiashara huyo nguli ambaye hapendi Yanga iwe tegemezi kwa mtu mmoja, hivi karibuni aliichangia Sh.Mil200 katika hafla ya Kubwa Kuliko iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.


“Kuhusiana na usajili nipo tayari kusaidia kama viongozi watahitaji mchango wangu kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu japo kuwa nimekuwa nikisadia pia kimyakimya.


“Lengo ni kutaka kuiona Yanga ikifanya vizuri, hata hivyo nitafanya hivyo kama mpenzi na shabiki wa Yanga na siyo kwa sababu nyingine,” alisema Rostam ambaye anapambana kuhakikisha Yanga inasimama yenyewe na inarejesha hadhi yake kitaifa na kimataifa.


Uongozi wa Yanga kupitia kwa mwenyekiti wake, msomi Mshindo Msolla pamoja na makamu wake, Frederick Mwakalebela wamesisitiza kwamba Rostam ana mchango mkubwa ndani ya Yanga na ana mapenzi ya dhati.

“Tumepanga kukutana naye hivi karibuni ili tuweza kuzungumza na kuona ni jinsi gani tutashirikiana naye kuhakikisha Yanga inapiga hatua lakini pia kuwa na kikosi imara ambacho kitairudishia heshima klabu yetu ambayo hivi karibuni ilipotea,” alisema Msolla ambaye ndiye kiongozi msomi zaidi kwenye klabu na soka la Tanzania akifuatiwa na Cresentius Magori wa ambae ni CEO wa Simba.

NYOTA WA 10 ASAINI

Kiungo Balama Mapinduzi (pichani) jana alisaini mkataba wa miaka mitatu Yanga na kutimiza idadi ya wachezaji 10 wapya waliomwaga wino rasmi Jangwani.

Mchezaji huyo aliyeichezea Alliance msimu uliopita, aliiambia Spoti Xtra kwamba amejipumzisha jijini Dar es Salaam akatuliza akili tayari kwa mapambano ndani ya klabu hiyo inayooga noti kwa sasa. Alisema; “Nitapambana na naamini juhudi zangu ndizo zitanifanya nipate nafasi kwenye kikosi cha kwanza.”

Ameweka wazi kwamba hawahofii Fei Toto wala Papy Tshishimbi kwenye nafasi ya kiungo kwani nao ni waajiriwa kama yeye na mwisho wa siku kocha ndiye atakayeamua. Mapinduzi anakuwa mtu wa 10 kusajiliwa na Yanga hadi sasa ambapo tayari wameshawasajili ambao ni Issa Bigirimana ‘Walcott’, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo na Juma Balinya.

Wengine ni Lamine Moro, Selemani Mustapha, Abdulaziz Makame na Ally Ally. Makamu mwenyekiti wa Yanga, Mwakalebela ameliambia Spoti Xtra, kuwa wanachofanya sasa ni kumalizia usajili wao uliopendekezwa na kocha Mwinyi Zahera ambapo kesho Jumatatu wanaweza kumaliza zoezi hilo. “Tunachofanya sasa ni kumalizia usajili tu wa pale kocha Zahera alipotuambia.

Wikiendi hii tutakuwa tunakamilisha zoezi zima la usajili ambao Jumatatu tunaweza kutangaza kumaliza kabisa. “Usajili wa sasa wote ni wa wachezaji wa ndani pekee kwa sababu tumeshamaliza wale wa kimataifa na muda si mrefu napo tutamaliza ili tuanze suala la kambi,” alisema Mwakalebela na kusisitiza kwamba usajili huo wa dakika za mwisho utakuwa na kishindo cha aina yake.

Alisema kwamba wanakuja na sapraizi moja kwa mashabiki wa timu hiyo kwani wamedhamiria kufanya usajili wa aina yake kwavile wanashiriki mashindano mengi na makubwa ambayo wanataka kubeba yote.

MZANZIBARI KUSAINI

Yanga wako katika mazungumzo na kiungo mshambuliaji wa timu ya Zanzibar Heroes na Kagera Sugar, Kassim Khamis. Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Spoti Xtra limezipata zimedai kuwa muda wowote kuanzia sasa mchezaji huyo atamwaga wino wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo.

SOMA NA HII  EYMAEL WA YANGA AZIPIGIA HESABU POINTI TATU ZA RUVU SHOOTING NAMNA HII