Home Uncategorized YANGA KUTISHA AFRIKA NZIMA, HII NDIYO SABABU

YANGA KUTISHA AFRIKA NZIMA, HII NDIYO SABABU


ACHANA na Yanga mbovu ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, kwani ya msimu ujao itakuwa tishio kutokana na aina mpya ya usajili aliyokuja nayo Kocha Mkuu Mkongomani, Mwinyi Zahera.

Yanga mpya ya msimu ujao inatarajiwa kuwa ya kikosi kipana tofauti na msimu uliopita kutokana na mapendekezo ya wachezaji ambao kocha huyo amependekeza kusajiliwa katika kukiimarisha kikosi chake.

Timu hiyo hadi hivi sasa tayari imefanikisha usajili wa wachezaji kumi ambao wazawa ni Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Ally Ally na kutoka nje ya nchi ni Issa Bigirimana ‘Walcott’. Wengine ni Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Lamine Moro na Suleyman Mustapha.

Katika kuhakikisha msimu ujao wa ligi anakuwa na kikosi bora, kocha huyo aina yake mpya ya usajili aliyokuja nayo ni kusajili wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja kwa lengo la kuwa na kikosi kipana ili akikosekana mchezaji mmoja, basi mwingine anakuwepo kuziba nafasi yake.

Ally aliyesajiliwa wiki iliyopita akitokea KMC, yeye amesajiliwa kucheza beki wa kati, lakini kocha alimpendekeza kutokana na kumudu kucheza beki wa kulia na ndivyo kama ilivyokuwa kwa Ally Sonso ambaye tayari amesaini kuichezea Yanga na anachosubiria ni kutambulishwa pekee baada ya Afcon ambaye anamudu kucheza beki wa kati na pembeni kulia.

Balama naye aliyetokea Alliance United, anamudu kucheza nafasi zote za winga namba 7 na 11, pia nafasi ya kiungo mchezeshaji namba 8 na 10, achana na huyo, yupo Sibomana kutoka Mukura ya Rwanda, anayecheza namba 11 na ana uwezo wa kucheza 7 na 10.

Yupo, Bigirimana ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa APR ya Rwanda ambaye yeye naye anacheza nafasi zote za ushambuliaji lakini anayoicheza zaidi ni namba 7, 10 na 11.

Wengine ni Kalengo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao nje na ndani ya 18, anacheza namba 9, pia anamudu kucheza 10 pekee kama ilivyokuwa kwa Balinya aliyekuwa anakipiga Polisi Uganda na msimu uliopita alikuwa mfungaji bora Ligi Kuu ya Uganda.

Mnamibia, Urikhob aliyekuwa kipenzi cha Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems ambaye alipendekeza usajili wake kwenye timu hiyo kabla ya kuja kusaini Yanga, yeye nafasi yake anayoichezea ya asili ni 10, pia ana uwezo wa kucheza nafasi zote winga 7 na 11, hivyo msimu ujao Yanga watakuwa na kikosi kipana kitakacholeta ushindani.

“Kwenye mapendekezo ya kocha alisema kuwa hataki mchezaji wa namba moja, alisema kila mchezaji anayesajiliwa lazima awe na uwezo wa kucheza namba moja na zaidi, alitania kwamba hata kama angempata kipa anayeweza kucheza beki pia angemsajili,” kilisema chanzo cha uhakika.

Msimu uliopita, Yanga hawakuwa na kikosi kipana kutokana na kutokuwa na wachezaji wa ziada pale anapokosekana mmoja katika mechi na hilo liliwahi kujitokeza kwenye mchezo wa mwisho wa ligi walipokutana na Mbeya City na Haruna Moshi ‘Boban’ kuchezeshwa beki wa kulia, ni baada ya mabeki wawili, Juma Abdul na Paul Godfrey ‘Boxer’ kuugua malaria.

SOMA NA HII  MBWANA SAMATTA YUPOYUPO ENGLAND