Home Uncategorized WABUNGE PIA WAMEONYESHA UDHAIFU KUHUSIANA NA TAIFA STARS, HUU SI WAKATI WA...

WABUNGE PIA WAMEONYESHA UDHAIFU KUHUSIANA NA TAIFA STARS, HUU SI WAKATI WA MAKUNDI

*Wakati mwingine wasialikwe kambini wakati wa mashindano
Na Saleh Ally, Cairo
WABUNGE walitaka kumtoa roho CAG, kisa aliwaita dhaifu, tena aliyeongoza vita hiyo ambayo wao waliita ni dharau ni Spika Job Ndugai.


Huenda lilikuwa ni suala la matamshi akiwa na maana wao si imara, liliwaudhi hadi CAG akaitwa bungeni na kujadiliwa.


Leo, kama kweli lile lilikuwa ni kosa, nao wamerudia baada ya kuwaita wachezaji wa Taifa Stars ni dhaifu.


Kikubwa kilichowauma ni Tanzania kufungwa na Senegal kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya Afcon ikiwa ni mechi ya historia timu ya taifa ya Tanzania kurejea tena Afcon baada ya miaka 39.


Tanzania ilikuwa inacheza na kizazi kipya kabisa, kizazi ambacho hakikuwepo kwa maana ya kushuhudia Tanzania ikicheza Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1980 nchini Nigeria.


Vijana wameanza mechi ya kwanza dhidi ya timu bora na namba moja barani Afrika, yaani Senegal. Lakini mwisho wameonekana ni dhaifu na hawana afya.


Najua sisi Watanzania ni watu wenye nidhamu, wa kweli lakini waoga kusema ukweli wetu. Mimi ninaanza kwa kusema hivi, wabunge na spika Ndugai, hawastahili kukaribishwa tena katika kikosi cha timu ya taifa.


Wao wanaweza kuwa chanzo cha timu ya taifa kupoteza mchezo dhidi ya Kenya, wameshindwa kuwa wenye uwezo wa kung’amua mambo na badala yake wamefanya siasa katika timu ya taifa!


Wanajua Stars ina mechi mbili ngumu, ina nafasi ya kujirekebisha. Lakini bahati mbaya wengi wao hawajui ubora wa Senegal, ndio maana wakaweza kusema maneno yale yanayofanana na “kisu” kwenye mioyo ya vijana wa Stars.


Askari kama ni dhaifu, anaweza kuwa bora kama utampa moyo ukimuonyesha njia bora za kupambana kwa kumpa moyo zaidi. Mfano, waliowaita wachezaji wa Stars ni dhaifu au wasio na afya wanaweza kuwarejea afya hiyo ndani ya wiki mbili?


Stars ndiyo iliwafanya wao wafike pale kambini kwa kuwa imefuzu. Dhaifu au wasio na afta ndio wamewafanya wao kufika pale. La sivyo wasingekuwa na maneno ya kusema.


Kuwaita dhaifu ni kuonyesha hauko upande wao na inawezekana kabisa ni udhaifu pia wa wabunge kutokuwa makini katika kuchambua mambo kabla ya kuzungumza.


Wanajua thamani ya kikosi cha Senegal? Wanafahamu kuhusuana na wachezaji wa Senegal walipitia akademi zipi? Wanatambua kuhusiana na wachezaji wa Senegal wanatokea katika ligi zipi?


Hawa dhaifu waliotuvusha, wanatokea katika klabu zipi na ligi zipi? Inawezekana pia hawajui Tanzania iko katika nafasi ya ngapi na Senegal ni ya ngapi kwa ubora?


Baada ya kipigo cha mabao 2-0, makosa yameonekana na sasa ndio wakati wa kuyafanyia kazi na maoni yanapotolewa, basi yawe na mwongozo wenye lengo la kusaidia.


Kuna haja gani kusema maneno ya kukatisha tamaa ukijua vijana wako wanakwenda kupambana? Kwani wao wabunge wamewahi kuisaidia nini Taifa Stars labda kuboresha kile walichokiona?


Mwaka 2006, ndio ilikuwa mashindano yangu ya kwanza ya Afcon kuripoti, nakumbuka ilikuwa hapa jijini Cairo na nilitumia muda wangu mwingine na mbunge wa Chemba, Juma Nkamia. Wakati huo yeye alikuwa mtangazaji wa BBC.


Tulizungumza sana kuhusiana na siku moja Tanzania kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo. Angalia leo ni miaka 13, ndiyo imepata nafasi hiyo na ajabu Nkamia anasahau kuwa juhudi kubwa zimefanyika na kinachotakiwa ni kuendelea kuijenga timu yetu kwa kuwapa moyo na kama ukweli ambao hakika ni mzuri, lakini bado kuna maneno ya kuchagua kuzungumza kulingana na wakati.


Angalia kiongozi anayelilia salamu ya Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike, eti amekutana naye kwenye ngazi hata hajibu salamu zao, hili nalo ni muhimu katika ushindi wa Taifa Stars? Kwani Amunike akikubali salamu, Stars itashambulia kwa nguvu na kupata mabao?


Kama mnapenda kuheshimiwa, basi kama viongozi litakuwa ni jambo zuri sana nanyi mheshimu kazi za wenzenu na mjifunze pia ili kuepuka kuwa dhaifu kwa kulalama tu.


Ukijifunza, unakuwa imara na kama kuchambua jambo unaweza kulichambua kwa ubora kabisa kuliko walivyofanya wabunge ambao wamewashambulia wachezaji wetu wanaokwenda vitani tena.


Kukosea ni sehemu ya kujifunza sote tunalijua hili. Hivyo bila ya woga wala kuvuta maneno, wabunge wameshindwa kuonyesha wana nia ya kuisaidia timu zaidi ya kuivunja nguvu. Kama ingekuwa ninapewa nafasi ya kuamua, ningesisitiza, siku nyingine kukiwa na mashindano, wasialikwe kwenye kambi ya timu ya taifa ili maneno waliyozungumza, wakazungumzie bungeni.


Kingine, niwashauri wabunge. Mna kila sababu ya kuwa msaada kwenye michezo badala ya kuwa mnasubiri mambo yakiharibuka mnaanza kulaumu tu!


Bajeti za michezo zinapitishwa bungeni lakini ipo wapi inayoweza kuwasaidia wachezaji wa Stars kuwa imara kwa maana ya kusaidia soka au michezo mingine kuanzia kwenye akademi bora zilizojengwa kama zile za Senegal ambao mliowaona ni imara bila ya kujua rimara wao unatokana na nini!

SOMA NA HII  WACHEZAJI BONGO VIWANGO VYAO KUSHUKA IWAPO WATASHINDWA KUFANYA HAYA