Home Uncategorized ADHABU YA WARDA WA MISRI, BADO INABAKI NA UJUMBE KWETU

ADHABU YA WARDA WA MISRI, BADO INABAKI NA UJUMBE KWETU





Na Saleh Ally, Cairo
GUMZO kubwa la hapa Misri ni kuondolewa kwa kiungo Amr Warda katika timu ya soka ya taifa ya Misri.

Inakuwa vigumu kujua ukubwa wa suala hilo kwa hapa Misri kama utakuwa nje au mbali na nchi hii.

Kuna makundi matatu au zaidi kuhusiana na hilo, wale wanaoamini Warda anayekipiga nchini Ugiriki ameondolewa katika timu ya taifa kwa kosa dogo licha ya kutuhumiwa kumdhalilisha mwanamitindo Merhan Keller kupitia mtandao wa kijamii. Wanaona lilikuwa ni jambo dogo tu.

Wapo wanaunga mkono na kusisitiza aondolewe timu ya taifa milele lakini wengine wanawapinga wakiamini wanawake wanatakiwa kuheshimiwa lakini adhabu ni kubwa kwa Warda kwa kuwa ni mambo yake ya nje ya uwanja na bado hawana imani na msichana anayemtuhumu kama kuna ukweli alimuonyesha sehemu zake za siri kupitia mtandao wa kijamii akitaka wafanye ngono kupitia mtandaoni. Yeye amekanusha.

Hii imefanya hadi Mohamed Salah naye kujitokeza na kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisisitiza heshima kwa wanawake lakini akizungumzia alichokifanya Warda, kinaweza kubadilika huko mbele pale naye atakapokuwa amejifunza na kubadilika, hivyo adhabu si kwa ajili ya kukomoa. Kama atabadilika, basi apewe nafasi tena kama uwezo unamruhusu.

Haya yanaweza kuwa ni yao, lakini kwa kiasi kikubwa yanafikirisha kwamba wachezaji wanapaswa kuwa na nidhamu kwa kiasi gani.

Nidhamu si ile ya uwanjani pekee, kuwa kioo cha jamii ni kazi ngumu. Kuwa mwakilishi wa taifa ni kazi ngumu na ya mateso, ndiyo maana taifa la Misri, leo liko vitani lakini wanakubali kumuangusha askari mmoja sababu ya kuhakikisha suala la nidhamu linapewa kipaumbele.

Nidhamu ni mwongozo wa maisha ya mwanadamu. Hata kama tajiri au una akili kiasi cha kutisha, bado kama hauna nidhamu utaanguka.

Tunaweza kujifunza hilo kwa wenzetu kwa kuwa nidhamu ina ukubwa wake kwa maana ya upana wa jambo lenyewe. Najaribu kuwakumbusha hilo na kuwaonyesha jambo. 

Nakumbusha upande ule unapoambiwa wachezaji wetu hawana nidhamu hasa nje ya uwanja, unaweza kusema haya hayahusiani na uwanjani na nidhamu si muhimu.

Leo, watende mambo ambayo ni tuhuma za kimtandao. Unaona hatua kali zinachukuliwa kwa mchezaji ambaye baadaye atakuwa shujaa wa taifa hili kutokana na ubora wake.

Kwa Misri, wanapata hasara kwa kuwa baada ya mashindano kuanza hauruhusiwi kuongeza mchezaji mwingine zaidi ya wale 23, maana yake watabaki na wachezaji 22 na Warda ni muhimu sana kadiri michuano inavyosonga mbele. Lakini kwa kuwa nidhamu ni muhimu na imepewa kipaumbele, amesukumwa nje.

Jiulize hapo nyumbani angefanya jambo kama hili mchezaji yeyote, kocha angeamua hivyo ingekuwaje?
Lazima tuiheshimu nidhamu na kuiamini kwamba ni msingi na kwa kila anayetaka kufanikiwa, lazima kuipigania na kuisimamia.

Kitu cha pili, nimejifunza, watu kutofautiana ni suala la kawaida na kikubwa ni kuheshimiana kwa kuwa kila mmoja atakuwa na mawazo yake. Si ikitokea mtu ametoa maoni tofauti aonekane hana nidhamu au ni mtu mbaya.

Katika jamii ya wapenda mpira kwetu sisi Watanzania, anayekuwa na mawazo tofauti gumzo litakuwa “ametumwa”, hili ni jambo baya sana.

Hatuwezi kuwa sawa kwenye kila kitu, ikitokea hivyo ujue huo ni unafiki uliotukuka. Kupishana mawazo ni nyenzo ya maendeleo. Hapa Misri, wao wanapishana na kujadiliana na hakuna ugomvi wa kudharauliana.

Wanakwenda na huu mjadala wakiwa wanaamini tofauti kwa makundi, lakini mwisho suala litapatiwa mwafaka na watu watakuwa wamejifunza.

Wakati mwingine mtoa maoni anaweza kuwa anakosea sana lakini makosa yake yakawashitua kukumbuka jambo jingine ambalo ni muhimu sana.

Ingawa hakuwa sahihi, lakini mwisho anakuwa amesaidia. Hivyo kupitia hili la Warda, tujifunze ubora na thamani ya nidhamu kwa wachezaji na mpira wetu lakini maisha ya kawaida lakini tujifunze kuhusiana na mjadala unavyoweza kubadili mambo badala ya upande au mtu mmoja au kundi la watu kutaka kuonekana linajua kila kitu na halikosoleki.

Msisitizo wangu ni kuyatathmini kwa mapana yake mambo ambayo yanatokea hapa Misri na kujifunza kwa lengo la kuendeleza mpira wetu au jamii zetu ama maisha kwa jumla.

Upo msemo hapo kwetu unasema “maisha ni kujifunza”, na kweli kujifunza ni mchakato unaoendelea katika maisha ya mtu siku zake zote duniani.

Rafiki yangu mmoja aliwahi kusema kuwa hata siku ya kufa mtu hujifunza kwamba “ahaa, kumbe watu ndiyo hufa hivi!” mtu anajifunza hadi kukata roho jinsi kulivyo, kabla hujafikia hatua hiyo huwezi kujua.

Hivyo ni lazima Watanzania tujifunze kwa wenzetu. Hapa Misri kwa sasa kuna watu wa tamaduni tofauti kwa kuwa wamekusanyika watu kutoka nchi mbalimbali, ni lazima kuna mengi ya kujifunza. Basi tufanye hivyo kwa faida yetu na mpira wetu na maisha yetu pia.
Fin


AFCON 2019

Kundi A
Pld W D L Pts
1. Misri 2 2 0 0 6
2. Uganda 2 1 1 0 4
3. Zimbabwe 2 0 1 1 1
4. DR Congo 2 0 0 2 0 



Juni 21, 2019
Misri 1-0 Zimbabwe 5:00 Usiku

Juni 22, 2019
DR Congo 0-2 Uganda 11:30 Jioni

Juni 26, 2019
Uganda 1-1 Zimbabwe 2:00 Usiku

Juni 26, 2019
Misri 2-0 DR Congo 5:00 Usiku

Juni 30, 2019
Uganda vs Misri 4:00 Usiku

Juni 30, 2019
Zimbabwe vs DR Congo 4:00 Usiku 

SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA V YANGA LEO TAIFA, MANULA NDANI