Home Uncategorized KWA YANGA HII MJIPANGE!

KWA YANGA HII MJIPANGE!


AMA kweli Yanga sasa wameamua, kuelekea msimu ujao maandalizi yameanza mapema na lengo ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi bora katika michuano yote msimu ujao wa 2019/20.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa kwa kikosi chote kuwa fiti uongozi wa klabu hiyo umejipanga kikamilifu, kwa kuhakikisha unaweka kambi yake ya maandalizi ya msimu mpya nchini China, ambapo wachezaji wapya nao wataungana katika safari hiyo.

Msimu uliopita Yanga ilipitia katika hali ngumu ya kiuchumi, jambo lililoifanya kushindwa kwenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu huo nje ya nchi na kujikuta ikiishia Morogoro tofauti na ilivyokuwa kwa watani wao Simba, ambao wao walienda nchini Uturuki.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zilizothibitishwa na Makamu Mwenyekiti wao, Frederick Mwakalebela, zimeweka wazi kuwa wanatarajia kuweka kambi nchini China, ingawa kambi ya awali ya maandalizi itaanza Julai 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Lengo la kuanza kambi mapema ni mahususi kwa ajili ya kujiandaa na tamasha lao la Kilele cha Mwananchi litakalofanyika Julai 27, mwaka huu. Wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo hadi sasa ni Lamine Moro (Mghana) na Ally Ahmed Ally wote wakiwa ni walinzi, Viungo ni Abdulaziz Makame, Balama Mapinduzi na Patrick Sibomana raia wa Rwanda.

Washambuliaji ni Juma Balinya (Mganda), Mustafa Suleiman (Mrundi), Maybin Kalengo (Mzambia), Sadney Urkhob (Mnamibia) na Issa Bigirimana (Rwanda).

“Ratiba ya kambi ya maandalizi tangu mwanzo tulishajipanga kwenda nchini China, hivyo tunatazamia kufanya hivyo mara baada ya kocha wetu Mwinyi Zahera kurejea nchini kwani wasiwasi wetu unatokana na ratiba ya ligi kama itatoka mapema na kujua lini itaanza.

“Mnajua Julai 7 wachezaji watakutana kambini hapa jijini Dar, ili wapange na kocha na kama wataona wiki hizo zinatosha kusafiri basi tutafanya hivyo kwani tamasha la Kilele cha Mwananchi ni Julai 27.

“Tuna wasiwasi wa kumaliza tamasha na ligi kuanza, endapo ratiba ya ligi haitatubana basi tutasafiri, ikitubana tutabaki hapa hadi baadaye,” alisema Mwakalebela.

SOMA NA HII  KAGERE ANATAKIWA KWENDA ZAMALEK NA TP MAZEMBE, WAKALA WAKE AZUNGUMZA - VIDEO