*Yadaiwa ana uhusiano na Kocha Amunike,
ashitukia mchezo
Na Saleh Ally aliyekuwa Cairo
LEO ni sehemu ya tatu na mwisho
kuhusiana na timu ya soka ya Tanzania,
Taifa Stars iliyokuwa kambini jijini Cairo
nchini Misri kwa ajili ya michuano ya Kombe
la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon.
Taifa Stars ilipoteza mechi zake zote tatu za
hatua ya makundi kwa kufungwa mabao 2-0
dhidi ya Senegal, 3-2 dhidi ya Kenya na 3-0
kutoka kwa Algeria.
Stars ilikubali jumla ya mabao 8 na kufunga
mawili huku ikitoka imeambulia patupu chini
ya Kocha Emmanuel Amunike raia wa
Nigeria.
Katika makala mbili zilizopita, nilielezea
namna kulivyokuwa na tafrani kubwa katika
vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa
mechi dhidi ya Kenya. Wakati wa
mapumziko hakukuwa na muda wa
kubadilishana mawazo zaidi ya mzozo.
Kocha Emmanuel Amunike, alivurumisha
maneno ya dhaharu ikiwemo kumkebehi
beki Kelvin Yondani kwamba alikuwa
anacheza kama mwanamke.
Maneno kama hayo aliwahi kumtolea beki
Abdi Banda kabla ya michuano ya Afcon.
Wakaingia katika mgogoro mkubwa kwa
kuwa yeye hakuwa kama Yondani
aliyeamua kumwaga machozi.
Pamoja na Banda na Yondani, mwingine
aliyewahi kukutana na tafrani hilo ni kiungo
wa Azam FC, Mudathir Yahya ambaye pia
alielezwa anacheza kama mwanamke.
Hii imekuwa ikiwakera sana wachezaji hao
lakini wamejawa hofu kulizungumza hili kwa
kuhofia kuonekana hawana nidhamu.
Waliokashifiwa hata wenzao, wameonekana
kukerwa na hali hiyo kwa kiasi kikubwa
sana. Unaona mwisho mchezaji kama
Erasto Nyoni aliamua kutangaza kujiondoa
katika kikosi cha Taifa Stars kwa madai
umri wake umekuwa mkubwa, Yondani
naye akaamua kufanya hivyo.
Mwisho, wamerejea baada ya mkwara wa
mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini hii
haiwezi kuwa tiba ya mioyo yao.
Kama unakumbuka wiki iliyopita, tuliishia
pale ambapo mtu mmoja raia wa Misri,
anayedaiwa kuwa na ukaribu na Kocha
Amunike alifika katika kambi ya Stars katika
eneo la New Cairo katika Hoteli ya
LandaMark Helnan na kutamka mambo
yaliyoonyesha kutaka upangaji wa matokeo.
Raia huyo wa Misri amewahi kufika kambini
hapo kumjulia hali Kocha Amunike na
inaelezwa ni wakala wake. Alikuwa akijua
kama inawezekana Stars kufungwa mabao
mengi zaidi.
“Alisema kwamba dhidi ya Algeria, Stars
itafungwa lakini angetamani kuona mabao
mengi. Hivyo alikuwa akiuliza ili iwe hivyo
yeye afanye nini,
” kinaeleza chanzo.
Mmoja wa madereva waliokuwa
wanawaendesha viongozi wa TFF ndiye
aliyeanza kunitonya kuhusiana na hilo,
akisisitiza niwaeleze viongozi kwamba yule
si mtu mzuri kwa kuwa amemsikia
akizungumza maneno hayo Kiarabu.
Mimi niliwafikia baadhi ya viongozi wa TFF
na kuewaeleza hali hiyo, tayari walikuwa
wametangulia mbele yangu baada ya
kunieleza walikuwa wamemrekodi.
Walikiri kweli alifika na kuuliza hivyo,
akitaka msaada wa kuona Stars inafungwa
mabao mengi, nao wakamuwekea mtego na
kumrekodi. Juhudi zangu za kupata sauti
hiyo zilifeli baada ya wao kugoma kunipa.
Hata hivyo, walionyesha kuwa kwenye
taharuki kama mtu huyo alishirikiana na
Amunike au alikuwa na nia yake tofauti
wakidhani, huenda alitaka, kufanya hivyo
kwa mambo mawili.
Kwanza huenda ni mcheza kamari na
anashirikiana na kocha, lakini wakataka
kujiridhisha. Au pili, ni mhuni tu ambaye
alitaka Stars ifungwe mabao mengi zaidi,
TFF wachukizwe na hiyo hali na baada ya
hapo wamtimue Amunike ili alipwe rundo la
fedha ili naye afaidike.
Wakati naanza kuandika makala haya
nilielezea kuhusiana na Watanzania
tunavyoamini siri, tunaona kutosema
mambo yanayotukera ndiyo uungwana.
Ajabu, tunaweza kuyazungumza mambo
hayo pembeni kama hadithi za
kuhadithiana, bila ya kuangalia kuyaweka
wazi yanaweza kutusaidia kuangalia njia
sahihi.
Kule Misri, kambi ya Taifa Stars haikuwa
rafiki sana na hakukuwa na raha iliyo sahihi
kuhakikisha jeshi linakuwa moja.
Wako wachezaji mfano nahodha Mbwana
Samatta, walikuwa funguo muhimu ya
kupunguza maumivu kwa waliodhihakiwa
kurejea katika nguvu ya mapambano hata
kama haikuwa kwa asilimia mia tena.
Tufiche tunayoona tunaweza kuficha, lakini
ukweli tuuweke hadharani kuepuka siasa na
mambo ya kuzunguka ili kuusaidia mpira
wetu kwa kuwa kucheza Afcon baada ya
miaja 39, isiwe shimo la kuficha kila maovu
kama kigezo cha kutuliza kila baya.
MECHI ZA TAIFA STARS AFCON:
Vs Senegal 2-0
Vs Kenya 3-2
Vs Algeria 3-0
MWISHO.