Na Mwandishi Wetu, Songea
Huku mbio za baiskeli kwa afya katika Tamasha la Majimaji Selebuka linaloendelea mjini hapa zikitarajiwa kurindima kesho Jumamosi, joto limeanza kupanda baada ya washiriki mbalimbali kuanza kuwasili wakiwamo wale nyota waliotikisa kwenye mbio za mwaka jana.
Mbio za Baiskeli katika Tamasha la Majimaji Selebuka zitakuwa za Kilomita 100 zikianzia Viwanja vya Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na kwenda kugeuzia eneo la Liganga kisha kurejea kwenye viwanja hivyo, lakini safari hii lengo kuu ikiwa ni kuhimiza mazoezi kwa afya na sio ushindani kusaka tiketi ya kimataifa.
“Lengo kuu tangu kuanzishwa kwa tamasha hili ilikuwa ni kuuinua mchezo wa mbio za baiskeli, jambo ambalo tumefanikiwa kwa kiasi fulani, hivyo kwa sasa tumeamua kulenga zaidi kuhimiza ujengefu wa afya kwa wananchi kwa kuendesha baiskeli,” alisema Mratibu Mkuu wa Tamasha la Majimaji Selebuka.
Tayari bingwa wa Taifa mbio za Baiskeli, Masunda Duba kutoka Simiyu na mwenzake Boniphace Masunda wameishawasili huku wakali wengine kutoka Arusha, Manyara, Mbeya, Iringa na wenyeji Ruvuma wakitarajiwa kushiriki hapa muda wowote.
Akizungumza mara baada kuwasili, Duba ambaye pia ni bingwa wa mwaka jana, alisema amejiandaa vema na ni matarajio yake kuibuka mshindi japokuwa si mbio za ushindani ila zikilenga kuhimiza afya.
“Nashukuru Mungu tumefika salama, lengo kuu ni kuhakikisha natetea nafasi yangu. Mwaka jana ilikuwa mara yangu ya kwanza kushiriki mbio za Majimaji Selebuka hivyo changamoto zilikuwa nyingi, tofauti na sasa nalijua vizuri tamasha hili kubwa Kusini mwa Tanzania,” alisema Duba.
Ikumbukwe mwaka jana Duba aligeuka gumzo mbali na kutumia muda mfupi zaidi, saa 2:53.05 bali kushiriki bila vifaa vya michezo kama kofia ngumu, bila viatu huku akitumia baiskeli ya kawaida iliyopachikwa jina la ‘ya kwendea shambani’.
“Safari hii, nitatumia ya kisasa zaidi, nimekatazwa na wakuu wangu, wamenishauri kutumia hii (ya kimichezo),” aliongeza Duba.
Duba alifuatiwa na Boniphace Masunda pia kutoka Simiyu akitumia saa 2:54.21 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Ipiyana Mbogela kutoka Iringa aliyehitimisha kilomita 100 ndani ya saa 3:06.55.
Mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake ataibuka na kitita cha Sh. Milioni 1, wa pili 700,000 wa tatu 500,000 huku wa nne hadi kumi wakijipoza na Sh. 50,000 kila mmoja.
Tamasha la Majimaji Selebuka ambalo limeingia msimu wa tano mwaka huu huandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea Mississippi (So-Mi), linatarajiwa kufikia tamati kesho Jumamosi.