Home Uncategorized YANGA TAFADHARI MALIZENI HII HADITHI YA YONDANI…..

YANGA TAFADHARI MALIZENI HII HADITHI YA YONDANI…..

Na Saleh Ally
YANGA tayari ipo kambini mjini Morogoro kujiandaa na msimu mpya wa 2019/20, msimu ambao mashabiki wengi wa Jangwani watakuwa na matarajio makubwa.


Matarajio makubwa kwa kuwa sasa wanajua ndani ya klabu yao kuna mabadiliko makubwa, watakuwa na viongozi waliochaguliwa na si wale wanaokaimu baada ya waliochaguliwa kuondoka.


Wanajua Yanga iko katika mikono salama, kinachotakiwa kwa sasa ni wahusika kufanya kazi kwa juhudi kubwa kwa lengo la kuisaidia timu kuwa na mabadiliko makubwa.


Mabadiliko makubwa ni pamoja na kuondokana na matatizo mengi hasa msimu uliopita, kama unakumbuka Yanga ilikuwa ikiandamwa na neno “njaa” ambalo si jambo sahihi kwa klabu kubwa kama hiyo.


Hata neno “michango ya msaada” ambayo ilionekana ni ukombozi kwa wakati huo, halikuwa sawa kwa hadhi ya Yanga lakini kama klabu kubwa ilihitajika kuwa na uongozi bora na madhubuti ambao unaweza kupanga mipango endelevu badala ya hii ya muda mfupi.


Sasa Yanga ina uongozi ambao umechaguliwa na wanachama wake, una jukumu la kuhakikisha inakwenda kwa mwendo wake sahihi. Mwendo ambao utaifanya Yanga kuwa katika heshima yake na ubora unaotakiwa.


Wakati viongozi hao wanaingia madarakani, bila shaka watakuwa wamekutana na matatizo mengi ambayo wanapaswa kuyatatua ili mambo yaweze kwenda kwa mwendo ambao ni bora, ninaamini watakuwa wameanza kufanya hivyo.


Pamoja na hivyo, tumeanza kuona kuna moshi unatokea upande wao, hasa baada ya kuwepo kwa taarifa ya baadhi ya wachezaji kushindwa kuingia kambini kwa kuwa wanadai maslahi yao. Hili jambo limekuwa gumzo kwa muda mrefu sana.


Ndiyo maana nikaanza kwa kukumbushia kwamba wameingia na kuyakuta matatizo. Mfano wachezaji kama Andrew Vincent ‘Dante’, Juma Abdul na Kelvin Yondani wamekuwa wakidai kwa muda mrefu sana.


Sasa hili limeanza kuleta picha nyingine ambayo inaonyesha kuna mambo hayajatulia na vizuri viongozi wakaacha kutaka kulificha na badala yake kulishughulikia. Vizuri badala ya kutaka wachezaji waonekane wabaya, au waandishi wanaosema ukweli waonekane ni adui, basi uongozi ulimalize.


Wachezaji wa zamani ambao wamekuwa na madai yao ni lazima yatimizwe na viongozi wanapaswa kuyatimiza yale ambayo wanaona ni sahihi na wanadai. Kitu kikubwa lazima kuamini nao ni wanadamu.


Kwa Yondani na wenzake wamekuwa wakidai kwa muda mrefu sana. Wamefuatilia, wameahidiwa na wakaendelea kuitumikia timu, wanapaswa kulipwa kwa kuwa walionyesha uzalendo kwa muda mrefu sana.


Inawezekana kabisa wameshindwa kuweka kila kitu wazi, lakini kama wanadamu wanaweza kuwa wanachukizwa kuona wachezaji wapya wakisajiliwa na kulipwa stahiki zao wakati wao ambao wana madai ya muda mrefu na wameipigania timu hawajalipwa.


Utaratibu mzuri kabisa, nimeona hata Simba waliufanya. Kwanza unaanza kumalizana na ulionao na unaowahitaji ambao wana madai yao. Kama ni suala la mikataba, kabla ya wachezaji wapya, unaanza kumalizana na wenyeji kwanza.


Baada ya hapo mambo yakikaa sawa, unaanza sasa kuangalia unachotaka kuongeza kutoka nje. Hii inasaidia zaidi kuweka utulivu lakini hata kutengeneza umoja kwa ajili ya baadaye.


Nimeona timu kadhaa kukiwa na chuki kati ya wenyeji na wageni na hii ni kutokana na kujengeka kisaikolojia kwamba wenyeji wanapewa kipaumbele cha chini na wageni wanathaminiwa zaidi. Mwisho unaweza kushindwa kutengeneza timu yenye umoja sababu ya hisia tu.


Hivyo kwa uongozi unapaswa kuwa “very trick” katika kushughulikia mambo ya madai ili kufanya kuwe na umoja hata baada ya kuyamaliza. Kama uongozi hautakuwa makini, unaweza kutengeneza matundu na baadaye nyumba ikaanza kuvuja.


Unaweza kulipima hili kama mzazi mwenye watoto zaidi ya mmoja au mtoto kutoka katika familia yenye watoto zaidi ya mmoja. Mzazi anapaswa kufanya kila jambo asionekane ana upendeleo lakini watoto hupenda kuona haki sawa baina yao na kama kuna yule anayependelewa, basi kunakuwa na fitna na hata chuki huzaliwa na kusababisha mpasuko.


Ninaamini uongozi wa Yanga lazima utakuwa na nia njema ya kuhakikisha kuna utulivu. Basi kama ni kweli kina Yondani na wenzake wanadai na madeni yao yanatambulika na ya zamani, basi wasiuziwe tena maneno, nao ni wanadamu wanachoka, walipwe ili waendelee na kazi.

SOMA NA HII  BANGO LA YANGA LAZUA MJADALA ACHAMBUZI ASEMA HAYA