Winga wa Yanga, Mnyarwanda, Patrick Sibomana ambaye anaongoza kwa kufunga mabao kwa wachezaji wote wa Yanga msimu huu hadi sasa, ametoa kauli ya kibabe kuwa japo hajaweka idadi ya mabao maalum ambayo atafunga klabuni hapo lakini atatimiza suala hilo kila mara ambapo atapata nafasi ya kufanya hivyo.
Sibomana aliyesajiliwa na Yanga kwenye dirisha hili la usajili lililofungwa Julai 31, mwaka huu akitokea Mukura Victory ya Rwanda, kwa sasa ndiye mpachika mabao tegemeo wa timu hiyo akifunga mabao nane kwenye mechi tisa ambazo amecheza hadi sasa.
Winga huyo wiki iliyopita alifunga bao lake la nane kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. Mechi hiyo ilipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Sibomana alisema kuwa hadi sasa hajajiwekea namba maalum ya mabao ambayo atayafunga kwa msimu huu lakini atakachokifanya ni kupambana vilivyo kuhakikisha anafunga kwenye kila mechi ambayo atapata nafasi ya kufanya hivyo.
“Sijapanga idadi ya mabao mangapi nitayafunga hapa, hilo Mwenyezi Mungu ndiye anajua. Kitu kizuri ni kwamba nafurahia kufunga na kuisaidia timu yangu kupata matokeo kila mara ambapo tunacheza.
“Ujue mimi ni mshambuliaji hivyo nina jukumu la kufunga mara kwa mara, kwa hiyo nitafunga mabao kila pale ambapo itatokea nafasi ya mimi kufanya hivyo. Kitu kikubwa pia mashabiki watarajie kuona nikifunga zaidi,” alisema Sibomana.