Na Saleh Ally
BAADA ya timu kuwa zimecheza mechi mbilimbili tu, tayari kuna mshambuliaji ameshafunga mabao manne, ukiwa ni wastani wa mabao mawili kila mechi.
Wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo ni wa juu kabisa katika kiwango cha washambulizi bora wa kimataifa.
Mshambuliaji huyo ni Teemu Eino Antero Pukki mwenye umri wa miaka 29, anayekipiga katika kikosi cha Norwich City na sasa ana mabao matano akifuatiwa na Raheem Sterling wa Manchester City aliyepiga mabao manne na tayari ameanza kutabiriwa kwamba huenda atakuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England maarufu kama EPL.
EPL inajulikana kwa ugumu wake, ukatili wa mabeki wake na namna ambavyo mambo yanakwenda kwa mshambuliaji kufunga haliwezi kuwa jambo jepesi hata kidogo.
Msimu uliopita ambao Man City wamekuwa mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo, wafungaji bora walikuwa watatu na hii inaonyesha kweli kuna ugumu kwa kuwa ushindani uko juu sana.
Wafungaji bora hao wote walikuwa wanatokea katika Bara la Afrika na kila mmoja yaani Sadio Mane, Mohamed Salah na Pierre-Emerick Aubameyang walifunga mabao 22.
Mechi mbili tayari Pukki ambaye anacheza EPL kwa mara ya kwanza baada ya Norwich kurejea tena, tayari ana mabao manne mkononi ikiwa ni tofauti ya 18 na waliyofunga akina Salah, Mane na Aubameyang kwa msimu mzima uliopita.
Swali ni kwamba Pukki raia wa Finland ataweza kwenda na kasi yake ya upachikaji mabao na kumfanya kuwa mfalme mpya wa kucheka na nyavu huko England?
Inawezekana kabisa Pukki akafanikiwa kuwa mfungaji bora bila ya kujali Norwich itafanikiwa kuwa moja ya timu bora au la. Lakini inaweza kukawa na ugumu kwake kufanikiwa kubeba kiatu cha dhahabu cha EPL. Kwa nini?
INAWEZEKANA
Aina ya ufungaji:
Kama umeona mabao manne ya Pukki, yanaweza kukupa jibu la hiki ninachokieleza kwamba ana kipaji cha aina yake.
Anapokuwa ndani ya eneo la 18 ni mtulivu sana, pia anajua mpira anaoupiga uende wapi. Kwa mabao manne ya EPL aliyofunga yanaonyesha anajitambua katika suala la umaliziaji.
Kikubwa ambacho amebakiza ni kudumisha hali hiyo ya ubora wa umaliziaji. Kama atafanikiwa katika hilo kufikisha mabao zaidi ya 20 kwake haliwezi kuwa jambo gumu sana.
Miguu:
Sifa kubwa ya miguu yake ni kuachia bunduki kali. Anaweza kupiga mashuti kutoka kushoto na kulia lakini anaweza kufunga zaidi akiwa nje ya 18.
Sifa nyingine nzuri ya miguu ya Pukki ni kufunga kwa kuunganisha mipira ambayo inakuwa haijatua. Hii inamfanya kuwa mmoja wa washambulizi wanaoonekana watasumbua kwa kuwa uwezo huo wanao washambulizi wachache sana.
Pamoja na hivyo, ana uwezo wa kupiga mashuti ya chini kwa aina ya utelezesho ambayo asili yake ni ubora wa kipimo kutoka kipa aliposimama na mpira unapokwenda.
Hii inamfanya kuwa mshambulizi mgumu kukabika kwa kuwa haujui atapiga wakati upi, mguu gani na kwa aina ipi!
Morali:
Kumbuka Pukki ndiye mchezaji bora wa Norwich kwa msimu uliopita akiwa mchezaji aliyetoa mchango mkubwa na kuisaidia timu yake kurejea EPL baada ya misimu kibao ya kubaki “ubaoni”.
Hii kwake ni morali inaweza kumfanya kujituma zaidi na kwa kuwa ameanza kufunga mabao harakaharaka, anaweza kupambana na kuweza kuendelea kufunga.
Mfungaji Bora:
Kuna nafasi kubwa kwake kuendelea kufunga kwa kuwa inaonyesha wazi kuwa ana uwezo mzuri wa kufunga mabao ndiyo maana msimu uliopita, amekuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza baada ya kufunga mabao 29.
Kawaida Ligi Daraja la Kwanza England maarufu kama EFL Championship, inaaminika ina ugumu zaidi na kuibuka mfungaji bora huko lazima uwe hatari na matata kweli.
HAIWEZEKANI:
Utofauti:
Ameonyesha anaweza kufunga mabao manne katika mechi mbili, lakini bado tunahitaji kusubiri tuone kama anaweza kuitawala EPL kirahisi kutokana na utofauti wake.
Wakali wengi:
EPL ina ushindani sana na unajumuisha timu nyingi vigogo kukiwa na wakali wengi wanaochuana.
Maana yake licha ya kupata uelekeo mzuri mapema, lakini bado kuna wengine kama akina Salah, Mane na Aubameyang hawawezi kulala badala yake watachuana naye vikali tofauti na ushindani wa Ligi Daraja la Kwanza.
Kiwango cha mabeki:
Katika mabao yake manne, moja amewafunga Liverpool. Moja ya kikosi bora katika ulinzi katika EPL ni Liverpool lakini ameweza kufunga bao.
Maana yake, anaweza kufanya vizuri lakini kuna kila sababu ya kumpa muda kwa kuwa mabeki wa EPL wana uwezo ulio juu zaidi.
Swali lilikuwa ataendeleza ubabe wake dhidi ya Chelsea, mechi iliyochezwa jana. Pukki kaonyesha hana utani, kwani alifunga bao lake la tano licha ya Norwich kupoteza mchezo kwa mabao 3-2 wakiwa nyumbani.
Maana yake katika mechi tatu, tayari Pukki ana mabao matano na amefunga mawili dhidi ya timu vigogo, yaani Liverpool na Chelsea. Huyu si mtu wa mchezo.