Home Uncategorized MWAMUZI HUYU NA TABIA ZAKE, ANANIPA HOFU YA LIGI KUU BARA ITAKAVYOKWENDA

MWAMUZI HUYU NA TABIA ZAKE, ANANIPA HOFU YA LIGI KUU BARA ITAKAVYOKWENDA



MKURUGENZI TPLB, BONIFACE WAMBURA




NA SALEH ALLY
NIKO katika Kundi la Mtandao wa Whatsapp ambalo linajumuisha wadau wengi sana wa mchezo wa soka.

Wadau kwa maana ya waandishi wa habari, waamuzi, wapenda soka, viongozi wa timu mbalimbali za soka ambao wamekuwa wakitoa mawazo yao kuhusiana na maendeleo ya mchezo wetu.

Wadau hao wamekuwa wakichangia mambo mbalimbali kutoka katika pande mbalimbali za nchi yetu kuhusiana na mpira.

Wakati mwingine mijadala ni kuhusiana na mpira hapa nyumbani lakini hata nje ya nchi kwa kuwa wako wanaounga mkono timu hizi na zile.

Katika moja ya mambo ambayo yamekuwa yakinishangaza katika kundi hilo ni kuhusiana na mtu mmoja ambaye ni mwamuzi aliye katika listi ya waamuzi wasaidizi wa Ligi Kuu Bara kuwa shabiki kindakindaki wa timu moja.

Mwamuzi huyo amekuwa akishangilia timu moja inayoshiriki Ligi Kuu Bara, bahati mbaya kabisa amekuwa akionyesha wazi katika kundi hilo.

Pale inapotokea timu hiyo kukosolewa amekuwa na hasira sana lakini amekuwa akizibeza timu nyingine dhidi ya timu anayoipenda. Mfano msimu uliopita mwishoni kabisa alikuwa akiibeza timu moja.

Siku chache baadaye nikamuona akiwa Mbeya anachezesha mechi ambayo ilikuwa ikicheza timu aliyokuwa akiibeza katika kundi lile la masuala ya mpira. Hii ilinishangaza sana.

RAIS WA TFF, WALLACE KARIA


Kwangu imekuwa ni wakati mzuri kuanza kuwazungumzia waamuzi wa Ligi Kuu Bara kupitia mwamuzi huyo ambaye ninasema amenishangaza sana.

Kila mmoja wetu ana haki ya kuwa huru na kushangilia kile anachoamini kinamvutia. Lakini kazi nyingine ikiwemo ya uandishi inatakiwa kukuondoa kuwa na mapenzi ya wazi kwa kuwa hautakiwi kuwa hivyo ili kupata nafasi ya kutenda haki.

Kushabikia hadharani bila ya woga tena kwa mtu ambaye unashiriki ndani ya uwanja au ni sehemu ya mchezo hili ni tatizo kubwa linaloweza kuleta hisia ambazo zinaonyesha kuwa kumbe wako waamuzi ambao hufanya mambo kwa kiwango duni wakiwa wamekusudia.

Mwamuzi huyu binafsi kwa tabia zake ingawa yeye anaamini watu hawajui yeye ni mwamuzi, hafai kabisa kuwa mwamuzi wa kiwango cha kuamua michezo ya ligi kuu kwa kuwa ana kila vimelea vya kutotenda haki kwa baadhi ya timu.

Mwamuzi wa aina hii ni mwepesi kushawishika kuchukua rushwa, mwamuzi wa namna hii hafai kuwa mtaalamu upande wa mchezo wa soka, badala yake anapendeza kubaki kama shabiki tu.

Kwa waamuzi wengine nao wanapaswa kujiepusha kutoka katika mfumo wa maisha laini ambayo yanaweza kuwafanya wawe mashabiki utafikiri wale wanaokaa jukwaani au walio tayari kushawishika kuchukua fedha na kuvuruga sheria 17 za mchezo wa soka.

Kuna kila sababu ya kuwa na tathmini ya mwamuzi mmojammoja ambaye kila mwamuzi ajifanyie tathmini kwamba kiwango chake kilikuwa vipi msimu uliopita na kipi alifanikiwa pia alichopungukiwa ili kufanya maboresho.

Anapoboresha kazi zake mwamuzi mmoja maana yake atasaidia waamuzi kuwa na viwango bora na baadaye kutengeneza timu ya waamuzi bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ligi Kuu Bara inahitaji waamuzi bora ili iwe na uamuzi sahihi, ili iwe na ubora unaotoa matokeo yanayopatikana kwa haki na si mapenzi binafsi ya watu au tamaa za watu binafsi.

Mwamuzi kama yule niliye naye katika kundi hilo la Whatsapp ni sumu kwa mpira wa Tanzania. Waamuzi wenye tamaa pia ni tatizo kubwa sana na msimu uliopita kulikuwa na malalamiko ambayo kama yatakuwa yamefanyiwa kazi basi itasaidia kuimarisha na kuupeleka mpira wa Tanzania juu zaidi.

Kama hakutakuwa na lolote lililofanyika, basi ligi itaboreshwa katika mambo mengi lakini mwishowe, tutaendelea kubaki palepale kwa kuwa na ligi yenye makossa rundo kwa faida ya wachache, jambo ambalo haliwezi kuwa maendeleo ya mpira wetu. Tubadilike.
SOMA NA HII  YONDANI NA YANGA MAMBO BADO