Home Uncategorized ZAMBIA SI SALAMA KWA YANGA, MECHI YA DAR VS ZESCO NDIO YA...

ZAMBIA SI SALAMA KWA YANGA, MECHI YA DAR VS ZESCO NDIO YA KUMALIZA KAZI


NA SALEH ALLY
UKIAMUA kuzungumzia rekodi kati ya timu za Tanzania dhidi ya zile za Zambia zinapokutana katika michuano ya kimataifa, ukweli umenyooka sana, kwamba Wazambia wanaonekana kuwa juu zaidi.

Wazambia hawakuwa tishio sana kwa Tanzania hasa katika miaka ya 1970. Walikuwa wakiihofia timu ya taifa ya Tanzania na timu zake za klabu. Huenda uoga wao uliwasaidia

Inawezekana uoga wa Wazambia, mwisho uligeuka kuwa ukombozi kwao kwa kuwa walijipanga na kujiandaa vilivyo ikiwemo kukuza vijana kwa muda mwingi ambao baadaye wakawafanya kuwa tishio wakiongozwa na nyota kama akina Numba Mwila, Moses Chikwalakwala na wengine waliokwenda kuuwawa katika ajali ya ndege.

Pamoja na hivyo, ikaonekana walikuwa na hazina kubwa kwani Kalusha Bwalya aliendelea kuongoza kizazi hicho kiendelee kuwa tishio na leo unaona Zambia ni moja ya vigogo vya soka Afrika.

Jirani zetu hawa, hakika wamepiga hatua na tunapaswa kukubali na kuendelea kujifunza kwao wakati huu.

Rekodi zao, zisiwe ukuta wa kutufanya tusifanye yaliyo sahihi ikiwezekana kutaka kuzipindua ili kuelekea kwenye ubora. Kuwa bora lazima umshinde anayeaminika ni bora zaidi yako.

Yanga inakwenda kukutana na Zesco na mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza imepangwa kupigwa Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Zesco ni moja ya timu bora kabisa za Zambia kwa kipindi hiki. Imekuwa bora kwa muda mrefu sasa kwa kipindi cha mika 10, ndio moja ya timu bora za nchi hiyo.

Kama timu inakuwa bora kwa muda mrefu ndani ya Zambia, hakuna ubishi kuwa timu hiyo ni bora hasa.

Kikubwa ni kukubali ubora wao lakini kukataa kuamini hawafungiki kwa kuwa hakuna timu isiyofungika duniani. Lakini kumfunga aliye bora lazima uwe bora zaidi. Kama Yanga watakubali wanakwenda kukutana na moja ya timu bora Afrika, basi lazima wawe na maandalizi bora ya vitendo na si maneno na kelele pekee kwa kuwa kufanya hivyo wataanguka.

Haiwezekani Zesco ionyeshe Zambia, isiwe bora itakapokuja Tanzania. Kuweka tahadhari na kucheza kwa juhudi na maarifa, itakuwa ndio dawa ya Tanzania.

Yanga hawana sababu ya kuona shida kujifunza kwa Simba ambao waliing’oa Nkana FC, moja ya timu bora za Zambia. Hii ilikuwa baada ya wao kupoteza kwa bao 2-1 ugenini na kuibuka na ushindi wa 3-1 nyumbani.

Safari hii Yanga wanaanzia nyumbani, maana yake mchezo wao wa Dar es Salaam unatakiwa kuwa unaotoa majibu kabisa. Kwamba wapate ushindi mzuri, ikiwezekana bila ya kufungwa hata bao moja. Haitakuwa kazi rahisi lakini kwa juhudi na maarifa inawezekana.

Ukiangalia mechi ya Yanga dhidi ya Township Rollers ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, unaona hasa kipindi cha pili Yanga ilikuwa na pumzi na stamina ya kutosha kuendelea kupambana angalau hata dakika 30 baada ya mechi kwisha.

Hii iliwalazimisha Rollers kurudi nyuma wakiwa wamejipanga kimaliza mechi hiyo kwa Botswana, lakini Yanga wakawaonyesha kazi.

Hivyo Yanga lazima wajipange wakijua mchezo wanaoanza nao ndio faida kubwa kwa kuwa ndio utakaoamua matokeo ya mechi inayofuata.

Yanga ijue kazi ni ngumu ambayo kama ubora utatangulia inawezekana na hakuna sababu ya kuuchukulia mchezo huo kama kitu chepesi tu kwa kuwa itakuja na Kocha George LWandamina ambaye si mgeni kwa Yanga.

Lazima kuhakikisha ni mapambano hasa na majibu mazuri yaanze kutengenezwa Dar es Salaam kwanza.
SOMA NA HII  YANGA YAPANGUA FITNA