KOCHA wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amemtaka straika wa Liverpool, Mohamed Salah kuacha uchoyo wakati akiichezea timu yake.
Kauli ya Wenger imekuja siku chache baada ya Sadio Mane kukorofishana na Salah baada ya kunyimwa pasi wakati akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga kwenye mechi dhidi ya Burnley.
Wenger, ambaye aliinoa Arsenal kuanzia 1996 hadi 2018, alidai kuwa Salah ameweka akili yake katika kuwaza ufungaji bora na kujikuta wakati mwingi ikiathiri kwenye maamuzi yake ya uwanjani.
Ulipotokea mzozo kwenye mechi ya Burnley ilibidi Jurgen Klopp atoe ufafanuzi juu ya suala hilo na kudai lilikuwa tukio dogo. Katika mchezo huo, ambao Liverpool iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Mane alikasirishwa na hatua ya Salah kutompa pasi wakati alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga.
Mane alifoka vikali uwanjani kiasi cha kumlazimisha Klopp amtoe uwanjani staa huyo.
Wenger alisema kuwa Salah anatakiwa kujifunza kutoka kwa staa wa Barcelona, Lionel Messi. “Salah anapaswa kuiga mfano wa Messi wa kufunga na kutoa pasi kwa wenzake,” alisema Wenger, ambaye kwa sasa hana timu ya kufundisha.
Wenger alisema kuwa tatizo la Salah ni kuwa kila mara anapokuwa na mpira kwenye eneo la timu pinzani anawaza afunge mwenyewe. Aliongeza kuwa Salah akipunguza uchoyo basi ana nafasi ya kubwa ya mwanasoka bora duniani.