Home Uncategorized ISHU YA MADAWA YA KULEVYA, HARMONIZE APEWA ONYO

ISHU YA MADAWA YA KULEVYA, HARMONIZE APEWA ONYO


ONYO! Kama mkali wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’ atakuwa ameanza mchezo mbaya wa matumizi ya madawa ya kulevya ‘unga’, basi mashabiki na wadau wakubwa wa burudani wamempa onyo na kumtahadharisha asije akapotea kwenye ramani, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lina mchapo kamili.

ISHU YAANZIA KWENYE PICHA

Onyo hilo limekuja kufuatia mkali huyo kutupia picha yake kwenye ukurasa wake wa Instagram ikiwa inamuonesha akivuta sigara iliyoaminika kuwa ni ile ‘kubwa’ ambayo hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

GUMZO KAMA LOTE

Baada ya kuposti picha hiyo ndipo gumzo kama lote likaibuka ambapo wengi walionekana kuitilia shaka sigara hiyo na kumtaka awe makini maana kama ameanza kutumia kilevi hicho ni dhahiri kwamba anakwenda kutumbukia shimoni.

“Awe makini sana na madawa ya kulevya, madawa hayajawahi kumuacha mtu salama, leo atavuta bangi, kesho atahamia kwenye cocaine, heroin na madawa mengine ya kulevya na watu watamsahau kabisa kama kuna mtu kama yeye,” alichangia jamaa aliyejiita Kijo kwenye Instagram.

MDAU ANENA

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mdau mkubwa wa burudani Bongo ambaye anamfahamu vizuri Harmonize, alisema Harmo anatakiwa kukaa mbali kabisa na madawa ya kulevya kwani ndiyo yaliyowakwamisha mastaa wengi ndani na nje ya Tanzania.

“Wewe kama unakumbuka kuna mastaa wengi sana tumeshawazika ambao walikuwa wanatumia hivyo vitu, nimesikiasikia mitandaoni akihusishwa na hayo mambo ya madawa. Hivyo nimhusie tu mdogo wangu kukaa nayo mbali kama itakuwa kweli ameanza kuyatumia,” alisema mdau huyo na kuongeza; “Madawa ya kulevya ni kifo, mdogo wangu Harmonize anapaswa kukaa mbali kabisa.”

STRESI ZATAJWA

Aidha, chanzo makini kilichopo Sinza-Kijiweni jijini Dar zilipo ofisi za Harmo, kimemtilia shaka Harmo kuwa huwenda siku hizi ana stresi na pengine zinaweza kuwa chanzo cha yeye kujiingiza kwenye ulevi wa madawa ya kulevya.

“Siku hizi tunamuona kama vile ni mtu wa mawazo sana, sasa ukishakuwa na mawazo ni rahisi sana kujikuta umeingia kwenye mambo ya hovyo,” kilisema chanzo hicho.

MENEJA WAKE ACHARUKA

Meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ alipoulizwa kuhusiana na mwanamuziki wake kuhusishwa na masuala ya madawa ya kulevya au poda, alicharuka ile mbaya na kusema kuwa watu waache kuzungumzia vitu negative (hasi) tofauti na hali halisi ya maisha ya mtu yalivyo.

“Waache bwana, kwa nini watu hawapendi kuongelea mambo ya msingi?” Alihoji meneja huyo akionekana kukerwa na ishu hiyo.

AZIDI KUTIRIRIKA

Meneja huyo alisema kuwa, Harmo hawezi kufanya mambo ambayo hayaipendezi jamii na kwa asilimia kubwa wanaitambua tabia ya Harmo.

“Kama kuna watu ambao wanasema ile picha ambayo ameiposti ni kwamba kwa sasa Harmonize yupo Nigeria, anatengeneza video ya nyimbo mpya kwa hiyo ile ni kava tu, lakini utakuta watu wanazungumza vibaya wakiona mwanamuziki katupia picha kwenye ukurasa wake si sahihi.

“Harmo hajajiingiza na yupo vizuri na hawezi kujiingiza huko na watu wapate elimu kwamba yule ni mwanamuziki kwa hiyo ikiwa ameweka picha yake yoyote wasiijaji, wanatakiwa wajue ni kazi anafanya,” alisema meneja huyo.

TUJIKUMBUSHE

Mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda alimuagiza Harmo kwenda kuripoti kituo chochote cha Polisi mara tu akitua nchini baada ya kusambaa kwa picha zilizomuonesha akivuta kitu kilichodhaniwa ni bangi akiwa nchini Nigeria. Hata hivyo, haikufahamika ishu hiyo imeishaje.

Miongoni mwa wasanii hao ni pamoja na Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ na Aboubakar Katwila ‘Q Chillah’. Chid alitumia na kujikuta akipotea kwenye ramani na hata alipotaka kurudi katika hali ya kawaida, mambo yamekuwa magumu sana.

Kwa upande wake Q Chillah, yeye alikiri kutumia kutokana na kutingwa na mawazo (stresi) na kwamba yalimpotezea sana muda wake kwenye gemu, lakini hata hivyo aliamua kuyaacha na sasa yupo vizuri anaendelea na muziki.

Pia mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ naye alikiri jambo hilo kumtoa kwenye ramani ya muziki kabla ya kuamua kuacha na bado anajikongoja.

Mbali na hao, wengine walijikuta wakitangulia mbele ya haki ilhali bado wakiwa vijana wadogo na muziki wao ukiwa bado unapendwa.

KUTOKA KWA MHARIRI

Kama Harmo atakuwa anatumia madawa ya kulevya, kupitia maonyo haya aliyopewa na watu wanaompenda, basi ni vyema akaachana nayo kwani ipo mifano mingi ya wanamuziki ambao walitumia madawa hayo na kujikuta wakiangamia.

CHANZO: IJUMAA WIKIENDA
SOMA NA HII  MARAIS HAWA KUISHUHUDIA SIMBA VS AL AHLY