Akiwa na siku nane tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa Yanga, Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Luc Eymael raia wa Ubelgiji amesema kwamba atatumia mifumo mitatu tofauti katika kikosi chake.
Mbelgiji huyo alitua nchini Alhamisi iliyopita na kuanza kibarua chake akichukua mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera ambaye alivunjiwa mkataba Novemba mwaka jana ambapo aliiacha timu hiyo kwa kaimu kocha mkuu Charles Mkwassa.
Mbelgiji huyo ameliambia Championi Jumatano, kuwa ndani ya kikosi hicho atatumia mifumo mitatu ambayo ni 4-2-3-1, 4-3-3 na 4-1-4-1, huku akibadilisha mtindo wa ushambuliaji ambapo anataka wacheze kwa haraka zaidi.
“Napendelea zaidi kucheza kwa mifumo mitatu nikiwa hapa Yanga ambayo ni 4-2-3-1, 4-3-3 na 4-1-4- 1, ambapo pia katika hilo nataka eneo la ushambuliaji licheze kwa spidi na haraka zaidi.
“Mifumo hiyo itategemea na aina ya mpinzani ambaye tutakutana naye tucheze vipi, lakini hiyo ndiyo mifumo ambayo tutakuwa tunaitumia kwa hapa,” alisema kocha huyo.