Mbwana Ally Samatta kila anakokwenda kucheza basi ujue Klabu ya Simba inaingiza mkwanja na hii ni kutokana na kuhusika kwenye malezi ya mshambuliaji huyo kabla ya kwenda TP Mazembe ya DR Congo.
Kwa sasa Samatta ameshakubaliana kujiunga na Klabu ya Aston Villa ambayo inashiriki Ligi Kuu ya England na jana alikuwa anakamilisha vipimo vya kujiunga na timu hiyo ya Uingereza, hivyo kama kawa, Simba inavuta mamilioni kibao.
Samatta anatarajiwa kujiunga na Aston Villa kwa dau la ada ya uhamisho la Euro mil 10 (Sh bil 25.4) akitokea KRC Genk ya Ubelgiji.
Kwenye dili hilo, Simba itaambulia kitita cha Euro 250,000 (zaidi ya Sh mil 635) kwa kuhusika kwenye malezi ya Samatta.
Wakati Simba wakipata kiasi hicho cha fedha, TP Mazembe wao watapata Euro mil 2.7 (zaidi Sh bil 6.8 ). Nitafafanua kwa nini, endelea kusoma.
Simba itapata fedha hizo kutokana na utaratibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao liliuweka kwa ajili ya kuzikumbuka timu ambazo zilihusika katika malezi ya mchezaji ‘solidarity contribution’ husika ambapo asilimia tano ya fedha ya mauzo yake hutolewa na kugawanywa kwa timu hizo.
Kutokana na hilo, asilimia tano ya euro mil 10 ambayo KRC Genk itamuuza Samatta kwa Aston Villa ni Euro 500,000, fedha hizo ndiyo ambazo Simba itaambulia ambapo itagawana nusu kwa nusu na TP Mazembe.
Akizungumza na Championi Jumamosi, aliyekuwa meneja wa Samatta wakati akiuzwa na Simba kwenda TP Mazembe na Genk, Jamal Kisongo alisema kuwa, fedha hizo ‘solidarity contribution’ ndiyo ambazo Simba itaambulia kutokana na mauzo hayo ya Samatta kwenda Aston Villa.
“Kwa hiyo hakuna fedha nyingine ambazo Simba watapata zaidi ya hizo. Unajua ni kwa nini? Hiyo ni kwa sababu viongozi wa Simba wakati wakimuuza Samatta, hawakuweka kipengele cha kugawana na Mazembe kiasi cha asilimia 25 ambazo wangepata kama Samatta atauzwa na KRC Genk kwenda timu nyingine.
“Kama viongozi hao wa Simba wangeliona hilo na kuweka kipengele hicho katika mkataba wao na TP Mzembe, kwa hiyo katika mauzo hayo ya Samatta kwenda Aston Villa nao wangepiga pesa.
“Wangegawana na TP Mazembe asilimia hizo 25 ya fedha ambazo watapata kutoka KRC Genk badala yake sasa wataambulia tu asilimia tano ya solidarity contribution,” alisema Kisongo.
Kwa maana hiyo, TP Mazembe itapata Euro mil 2.5 (zaidi ya Sh bil 6.3) kutoka KRC Genk ambazo ni asilimia 25 za mauzo ya Samatta kwenda Aston Villa kama atauzwa kwa dau hilo la Euro milioni 10, lakini pia itapata Euro 250,000 za solidarity contribution.
Kutokana na hali hiyo TP Mazembe itakuwa imejipatia jumla ya Euro mil 2.7 (zaidi ya Sh bililioni 6.8) kutokana na mauzo hayo ya Samatta.