LEO Januari, 22 macho na masikio ya mashabiki ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Namfua, uliopo mkoani Singida utakaoikutanisha Singida United na Yanga.
Kikosi cha Singida United kilicho chini ya Kocha Mkuu Ramadhan Nswanzurimo kitawakaribisha wageni wao Yanga iliyo chini ya Mbelgiji, Luc Eymael kweye mchezo wao wa kwanza msimu huu wa 2019/20.
Hii inakuwa ni mechi ya kwanza kwa Eymael kucheza nje ya Dar, baada ya mbili kucheza Dar alipoanza kupokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Kagera Sugar na kichapo kingine cha bao 1-0 mbele ya Azam FC Uwanja wa Taifa.
Mechi ya leo ina balaa zito kwa timu zote mbili kutokana na umuhimu wa pointi tatu ambazo timu zote mbili zinahitaji kutokana na haya hapa:-
Mwendelezo wa rekodi
Singida United haijawahi kuacha pointi tatu zipeperuke kirahisi mbele ya Yanga inapocheza Uwanja wa Namfua tangu ilipopanda daraja msimu wa mwaka 2017/18.
Mechi ya kwanza Singida United ililazimisha sare ya bila kufungana na Yanga na msimu uliofuata wa mwaka 2018/19 Singida ilikaza na kulazimisha sare ya bila kufungana. Kwa rekodi hizo Singida United itahitaji kushusha balaa lake kuzilinda huku Yanga ikipania kuzitibua jumla.
Kikombe cha kushuka daraja na ubingwa
Singida United imejiengua kwenye vita ya kikombe cha ubingwa ila ipo kwenye kikombe cha kupambania nafasi yake kwenye kuepuka kushuka daraja msimu huu kutokana na nafasi iliyopo kwa sasa.
Kwenye jumla ya mechi 16 ilizocheza imeshinda mechi mbili tu hivyo itapambana kuongeza idadi ya mechi za kushinda ili kujiongezea nafasi ya kubaki ndani ya ligi huku Yanga wao wakipambana kuingia kwenye kikombe cha kupambania ubingwa wa ligi.
Yanga ipo nafasi ya nane kwenye msimamo ina pointi 25 imecheza jumla ya mechi 14 ikiwa imeachwa kwa jumla ya pointi 16 na mpinzani wake Simba mwenye pointi 41 ikiwa imecheza mechi 16 hivyo leo Yanga itakuwa ikipambana kupunguza mlima wa pointi alizoachwa na Simba.
Balaa la wakongwe
Usajili wa dirisha dogo kwa Singida United umeongeza wakongwe ambao wanaitambua ligi vizuri ikiwa ni pamoja na Athuman Idd Chuji, Haruna Moshi ’Boban’ Haji Mwinyi hawa wote wanaitambua falsafa ya Yanga kwa kuwa walikuwa kwenye kikosi hicho kwa nyakati tofauti.
Balaa lao litanogeshwa watakapokutana na Mrisho Ngassa, Kelvin Yondani na Juma Abdul ambao nao wapo kitambo ndani ya Yanga.
Heshima ya pointi tatu
Mafahari wawili wanapokutana mmoja anaposhinda huwa heshima hasa akisepa na pointi tatu. Singida United wanatafuta heshima ya ushindi kwa mara ya kwanza mbele ya Yanga na Yanga nao wanatafuta heshima ya kusepa na pointi tatu mbele ya Singida ugenini.
Hesabu za makocha
Nswanzurimo wa Singida United alisema kuwa hana presha ya kukutana na timu kubwa kwa sasa kwani ushindi wake mbele ya Ruvu Shooting na usajili aliofanya unampa nguvu ya kupambana na timu yoyote.
“Kikubwa ninachotazama ni kuona namna gani nitatumia wachezaji ambao nimewasajili pamoja na wale ambao nilikuwa nao muda mrefu kupata matokeo. Sina hofu na ushindani kwani timu zote zipo sawa.
Eymael wa Yanga alisema kuwa uwezo mkubwa ambao wanao wachezaji wao na makosa ambayo amejifunza kupitia kwao yanawapa nafasi ya kupata matokeo.
“Kupitia makosa kwenye mechi zilizopita nimejifunza jambo na nimelifanyia kazi. Ni wakati wetu wa kuona namna gani tunaweza kupata matokeo kwenye mechi zetu zinazofuata.
Matokeo yao walipokutana
Zimekutana kwenye jumla ya mechi nne na jumla ya mabao manne yamefungwa ambapo, Yanga imefunga mabao matatu na Singida United imefunga bao moja pekee.
2017/18 Singida United 0-0 Yanga
Yanga1-1 Singida United
2018/19, Yanga 2-0 Singida United
Singida United 0-0 Yanga
2019/20 Singida – Yanga?