NA SALEH ALLY
KAMA utakuwa hauifuatilii Ligi Daraja la Kwanza unaweza ukadhani mambo ni rahisi, lakini ni moja ya ligi ngumu sana.
Utakuwa umeangalia mfano mzuri katika mechi za Kombe la Shirikisho la Azam Sports namna ambavyo timu za daraja la kwanza zimekuwa zikiwapa wakati mgumu wanaotokea Ligi Kuu Bara.
Timu nyingi za daraja la kwanza, zina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kupambana hata katika ligi kuu.
Wakati mwingine inakuwa nafasi haijapatikana wao kuonekana na kadhalika. Lakini wachezaji wengi wanakuwa na viwango bora kabisa, ndiyo maana tumeona hata timu kama Simba inayoonekana kuwa na wachezaji bora ikivuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho na timu ya daraja la kwanza.
Angalia mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, mabingwa wa Kombe la Shirikisho, Mtibwa Sugar wameng’olewa na timu ya daraja la kwanza ya Sahare All Stars ya Tanga.
Hii ni sehemu tosha ya kuonyesha kuwa Ligi Daraja la Kwanza kuna timu nyingi zenye uwezo bora kabisa.
Ubora wa uwezo unafanya kuwe na ushindani mkubwa miongoni mwa timu hizo zinapokutana zenyewe kwa zenyewe hasa katika ligi yao.
Kama unavyojua, sehemu kunapokuwa na ushindani kuna mambo mengi sana, yanaweza kuwepo mazuri au mabaya. Na mara nyingi wale ambao huzidiwa mbinu za kimchezo, hutumia mbinu mbadala ambazo si sahihi.
Kumekuwa na malalamiko mengi sana katika Ligi Daraja la Kwanza na mengi yamekuwa na msingi sana, huenda Bodi ya Ligi Tanzania imejisahau na kuelekeza nguvu nyingi katika Ligi Kuu Bara.
Leo nimeona niwakumbushe watu wa bodi kwamba wanaotokea Ligi Kuu Bara, huenda kupumzika Ligi Daraja la Kwanza na wanaopanda kwenda ligi kuu.
Hii ni sehemu nzuri ya kutambua umuhimu wa Ligi Daraja la Kwanza kama daraja muhimu la kwenda ligi kuu ambayo ndio sura ya nchi yetu.
Hivyo ni lazima iwe na viwango bora katika masuala muhimu kama waamuzi, vifaa kwa maana ya uwanja na sehemu sahihi inapochezwa lakini umuhimu wa ulinzi na mambo mengine.
Tumeona wachezaji wakionewa na baadhi ya timu sababu zinaongozwa na majeshi tu na Bodi ya Ligi ikakaa kimya bila ya kuchukua hatua yoyote.
Tumeona waandishi wakinyimwa ulinzi ambao ni sahihi kwa kuwa tu inaonekana huko ni mikoani au inayochezwa ni Ligi Daraja la Kwanza.
Mara kadhaa, tumeshuhudia waamuzi wakifanya madudu ya wazi kabisa bila ya hofu kwa kuwa wanajua tu hiyo ni daraja la kwanza lakini pia wamekuwa wakitumia vibaya ligi hiyo kutoonyeshwa kwenye runinga.
Si jambo sahihi kwa Bodi ya Ligi nayo kuyakalia kimya haya na inapendeza sana kuendelea kutoa adhabu kila inapowezekana na kuzitangaza ili wengine wote waliokuwa na nia mbaya wajue kwamba hakutakuwa na mchezo.
Pamoja na hivyo, pia si vizuri kusubiri adhabu tu, badala yake Bodi ya Ligi inapaswa kulifanyia kazi suala la mafunzo maridadi ya waamuzi, mameneja wa viwanja na wale wanaohusika na viwanja ili vitu vifanyike katika utaratibu sahihi wa mpira wa miguu.
Kama kutakuwa na marekebisho haya, ninaamini yatachangia ligi hiyo kuendelea kuwa imara na kufanya kila timu zinazopanda ziwe imara kweli na kutengeneza ushindani bora zaidi katika Ligi Kuu Bara ambacho ndio kipimo cha mpira wetu Tanzania.
Ligi Daraja la Kwanza isigeuzwe kichaka cha wahuni ambao wanataka kufanya madudu yao kupitia udhaifu unaendelea. Bodi ya Ligi boresheni upungufu, wekeni jicho lenu karibu ili kuimarisha na baadaye faida itakuwa kubwa maradufu.