Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kanda ya Kati kukumbwa na mvua kubwa kwa siku tano mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na mamlaka hiyo, mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Mara, Kagera, Geita na Tabora kwa Kanda ya Ziwa. Mikoa ya Kanda ya Kati itakayokumbwa na mvua hizo ni Singida na Dodoma huku mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwa Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Sambamba na mikoa hiyo, taarifa hiyo ilisema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Rukwa, Iringa, Mbeya na Njombe pia itakumbwa na mvua hizo. Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kusababisha uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo na makazi kuzungukwa na maji.
“Athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii,” ilisema taarifa hiyo.
Kutokana na hatari hiyo, TMA imewatahadharisha wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo, kuchukua tahadhari mapema na kujiandaa.