Home Uncategorized YANGA YAKIONA CHA MOTO KAMATI SAA 72

YANGA YAKIONA CHA MOTO KAMATI SAA 72


BALAA walilokutana nalo Yanga ni kupigwa faini ya shilingi milioni 2.7 kutoka kwa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya saa 72) iliyokaa Januari 20, mwaka huu kutokana na makosa mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto aliweka wazi kwamba kikosi hicho kimepigwa faini ya shilingi laki tano baada ya kutowasilisha listi ya wachezaji wake walipocheza na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Samora, Iringa Desemba 29, mwaka jana.

Prisons nao wamekumbana na faini hiyo kwa kuzingatia kanuni ya 14:3 juu ya taratibu za mchezo.

“Faini nyingine ya Yanga ni kutokana na mashabiki wao kurusha chupa uwanjani na kuwarushia waamuzi kwenye mechi yao dhidi ya Simba, Januari 4, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni 43:1 kuhusu udhibiti wa klabu.

“Pia Yanga wamepigwa faini ya shilingi laki mbili kwa kutotumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo, licha ya kulinda vyumba hivyo kwa siku tatu nzima. Kwenye mechi hii kuna matukio ambayo yalitokea na hayakuripotiwa, tutayapeleka kwenye kamati maalum, ambapo kwa faini hizo mbili wamepigwa rungu la shilingi milioni 1.2.

“Wachezaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, Ramadhan Kabwili na Cleophace Sospeter wamepigwa faini ya shilingi laki tano na kufungiwa mechi tatu baada ya kugoma kuingia vyumbani kwenye mechi yao na Mbeya City. Wachezaji wa Mbeya City Shaban Majaliwa na Kevin John nao wamekumbana na adhabu kwa kuzingatia kanuni ya 38:9 ya udhibiti wa wachezaji,” alisema Mguto.

Kwa adhabu hizo za Yanga wamepigwa faini ya shilingi milioni 2.7.

“Kocha wa Yanga, Luc Eymael amepewa onyo kwa kufanya vitendo na kutoa matamshi yasiyofaa juu ya masuala ya ubaguzi kwenye mechi yao na Azam FC, lakini pia tunawaagiza Yanga nao watoe tamko juu ya kocha wao huyo kutokana na suala hilo.

“Katika Ligi Daraja la Kwanza, Friends Rangers wamepewa pointi tatu na mabao matatu baada ya wapinzani wao Njombe Mji kuwa na wachezaji pungufu uwanjani.

“Njombe walikuja uwanjani wakiwa na wachezaji ambao hawakuwa wanafuzu kucheza katika mechi hiyo kwa sababu walisajiliwa dirisha dogo. Wakabaki wachezaji saba na bahati mbaya kipa wao akaumia akapelekwa hospitali wakawa sita wakashindwa kuendelea.

“Ligi Daraja la Pili, Mkamba Rangers wamepoteza mechi yao dhidi ya Villa Squad, baada ya kufanya udanganyifu wa leseni kwa kubandika sura za wachezaji wengine katika leseni za wachezaji wengine. Villa wamepewa pointi tatu na mabao matatu,” alisema.
SOMA NA HII  YANGA YAZITAKA POINTI TATU ZA NDANDA LEO TAIFA