PARIS, Ufaransa | STAA wa PSG, Neymar amekuwa akilalamikiwa sana kutokana na tabia zake za kuonekana anadanganya ili tu atimize jambo lake.
Neymar ni miongoni mwa wanasoka mabishoo duniani huku akiwa na visa vingi kati ya Februari na Machi ya kila mwaka.
Kwa takribani miaka mitano mfululizo, Neymar amekuwa akikosekana kwenye mechi za timu yake kati ya Februari na Machi, huku wachunguzi wa mambo wakisema kwamba amekuwa akifanya makusudi.
Imeonekena zaidi ya mara tano, kinapokaribia kipindi cha kusherehekea siku yake ya kuzaliwa au siku ya kuzaliwa kwa dada yake, basi lazima akosekane kwenye timu yake.
Neymar amezaliwa Februari 5, 1992, huku dada yake, Rafaella Santos akizaliwa Machi 11, 1996. Tangu akiwa Barcelona na sasa PSG, hali hiyo imekuwa ikiendelea.
Staa huyo wikiendi iliyopita aliamua kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na rafiki zake, huku akifanya sherehe hiyo siku moja baada ya kuumia uwanjani na kukosekana katika mchezo wa Jumanne ya wiki hii.
Kitendo cha kuripotiwa ameumia, kisha kufanya sherehe kubwa, kimewashangaza wengi.
Mbrazili huyo alisherehekea siku yake hiyo ya kuzaliwa jijini Paris, Ufaransa akiwa na baadhi ya wachezaji wenzake wa PSG akiwemo Edinson Cavani, Angel Di Maria, Mauro Icardi pamoja na winga wa Lyon, Memphis Depay, huku mavazi yao rasmi yakiwa ni nguo nyeupe.
Kwa kifupi, Neymar anapotaka kufanya jambo lake, hataki kuona ratiba zikiingiliana. Tazama alikosekana kwenye mchezo wa Jumanne ikionekana ni makusudi tu ili awe na muda mzuri wa kuandaa sherehe yake.