Home Uncategorized NAMNA KOCHA YANGA ALIYEIBUKA NYOTA WA MCHEZO KATIKA KARIAKOO DABI

NAMNA KOCHA YANGA ALIYEIBUKA NYOTA WA MCHEZO KATIKA KARIAKOO DABI




Na Saleh Ally
YANGA imeifunga Simba na kuwaacha wengi wakiwa hawaamini kilichotokea kwa kuwa ilionekana kuwa mechi hiyo ya pili ya Ligi Kuu Bara inayowakutanisha watani hao ilikuwa ni ya Simba kuonyesha kuwa watani wao walibahatisha, kwamba ilikuwaje Yanga wakapata sare ya mabao 2-2 katika mzunguko wa kwanza!
Kilichotokea Yanga iliyoonekana kubahatisha sare kuibuka na ushindi, ilionyesha kiwango
kizuri, jambo ambalo hata mashabiki wa Simba waliona kweli limetokea na wamethibitisha.
Baada ya mchezo huo, kukawa na kila aina ya gumzo kuhusiana na kilichotokea na zaidi
wachezaji akiwemo mfungaji wa bao pekee, Bernard Morrison wakawa wakizungumzwa kila kona.

Wachezaji walizungumzwa sana, mfano Metacha Mnata, Lamine Moro, Said Juma β€˜Makapu’, Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi, Feisal Salum β€˜Fei Toto’ na wengine kuwa walicheza vizuri na kuifanya Simba isionekane katika ule mwonekano uliozoeleka.

Wengi walifurahishwa na wachezaji na hata baadhi wakapishana kuhusiana na wachezaji kuwa yupi alikuwa nyota wa mchezo, Metacha, Molo, Tshishimbi au Morrison aliyeimaliza Simba kwa mkwaju wa faulo uliomaliza mechi kwa bao 1-0.

Binafsi nilikuwa na nyota tofauti kabisa wa mchezo ingawa alikuwa akichezea nje ya
uwanja. Huyu ni Luc Eymael ambaye
alisaidiana na Charles Boniface Mkwasa kuhakikisha wanafanya kilicho sahihi na wachezaji wao walipoweza tu kuuvaa mfumo,
basi kazi ikawa imeisha.

Viungo sita:
Yanga walianza na mfumo wa 3-5-1-1 ambao uliwafanya kuwa na wachezaji sita katikati ya
uwanja huku wakimuacha Ditram Nchimbi pekee kupambana akigongana na mabeki wa kati wa Simba.

Viungo sita kimfumo, unaona waliokuwa wakichezesha juu na chini ni Haruna Niyonzima, Tshishimbi, Mapinduzi, Fei Toto na Morrison hakufanya kazi ya kukaba, zaidi ilikuwa ni kusukuma mashambulizi juu kwa
kasi. Halafu Makapu akicheza namba tano, yeye ndiye alitumika kama kiungo wa chini
kutuliza timu.
Kila Yanga walipotaka kuanzisha mpira kwa kuwa kwa asili Makapu ni kiungo, walimuachia yeye aanze mpira chini, jambo ambalo liliwafanya Simba wapande juu na kuacha matundu katikati ya uwanja na kuwapa Yanga nafasi ya kucheza.

Kazi maalum:
Unaona kulikuwa na viungo sita lakini Eymael aligawanya makundi na karibu kila mmoja akawa na kazi yake maalum. Wakati Makapu ilikuwa kukaba mipira ya mwisho lakini alitakiwa kutuliza timu na unaona baada ya hapo Tshishimbi ikawa ni kukaba kwa nguvu lakini kuhakikisha viungo wa Simba hawachezi kwa uhuru kwa maana ya kuwabugudhi.

Bugudha hii kwa viungo wa Simba ilikuwa maalum kwa kuwa Yanga walikuwa wanakaba kwa nguvu na kuna mfumo ambao hutumiwa na timu nyingi za Ulaya, mfano Barcelona, timu inapopoteza mpira inatakiwa ndani ya sekunde 30 kuwa imeurejesha au kuutoa nje ya mchezo.

Hii ni kwa kuwa falsafa ya kimpira inaonyesha hivi, timu inapobaki na mpira zaidi ya sekunde 30, inaanza kujiamini na inaweza kutekeleza yale ambayo wamejifunza ya kimfumo kupata
matokeo.

Kama utawapokonya mpira ndani ya sekunde 30, maana yake wanakuwa hawajafikia kuanza kufanya utekelezaji sahihi, maana yake watalazimika kuanza upya tena, jambo ambalo wakikosea mara nne hadi sita,
wanachanganyikiwa.

Angalia ukabaji wa Tshishimbi, Makapu na Moro, ilikuwa utafikiri ugomvi lakini ulikuwa ni mpango maalum.

NAMBA SITA WAWILI:
Pamoja na kwamba ulikuwa ukiangalia kwenye listi, Fei Toto ni namba nane na Niyonzima namba 11, lakini hawa wote waliingia ndani na kucheza kama viungo wachezeshaji wakiwa huru lakini muda mwingi Fei Toto akacheza chini na Tshishimbi.

Huu ni mfumo mwingine bora wa ulinzi kama unakutana na timu yenye viungo wengi wenye
uwezo. Kunakuwa na namba sita wawili ambao wanacheza katika mstari mmoja. Mmoja anakuwa anakaba zaidi na mwingine ni kuchezesha lakini akishiriki ukabaji.


Niyonzima anaposhuka anakuwa kama namba nane, Morrison ambaye ni namba 10, anapata
nafasi kubwa au uwanja mpana wa kukimbia katika eneo lote la kushoto.

Ukiangalia mfumo huu ulikuwa ni wa kubana kuhakikisha Simba hawafungi bao na kujaribu
kama itawezekana kufunga bao na kama ikishindikana sare si mbaya.

Pamoja na hivyo, Eymael alipoona ameweza kuwadhibiti Simba, Yanga ikaanza kusukuma
mashambulizi mengi na hatari.

Ukiangalia timu za Waarabu, mfano Al Ahly, Esperance, Zamalek na nyinginezo hutumia mfumo huo wanapokuwa ugenini. Kawaida wanaanza mechi kwa kasi wakitaka kupata bao la mapema halafu wanatulia na kulinda wakifanya mashambulizi ya kushitukiza.


Kama wataona wapinzani wamezidiwa, basi wanaanza kushambulia mfululizo kuhakikisha wanapata mabao ya ugenini na Eymael alionekana wazi kumzidi kiufundi Mbelgiji
mwenzake, Sven Vandenbroeck ambaye ni kinda kwake kwa maana ya uzoefu.

Bado hakuna ubishi kwamba kweli Simba wana wachezaji wazuri, bora na wana uwezo hasa ndio maana unaona wanaongoza kwa mabao ya kufunga, imara wamefungwa mabao machache, wana pointi nyingi na ndio vinara wa ligi, lakini mambo yalikuwa tofauti katika mechi hiyo dhidi ya Yanga kwa kuwa Eymael ndiye aliteka shoo kwa kuwa nyota wa mchezo aliyekaa katika benchi.
SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA KITAKACHOANZA LEO DHIDI YA CHIPUKIZI