NA SALEH ALLY
AWALI ilikuwa ni dalili lakini sasa tunaweza kusema uthibitisho umebaki ni kufungua mdomo tu lakini kila kitu sasa kipo wazi.
Uwazi huo ni kwamba Singida United inateremka daraja kwa kuwa hali ilivyo, hakuna ubishi tena na juzi umeona, imefungwa mabao 8-0 na Simba na huenda hizi ziwe salamu kwa walioboronga akiwemo Mwigulu Nchemba.
Mambo yamekuwa magumu katika kikosi cha Singida United na sasa kama utapata nafasi ya kuzungumza na wachezaji wa kikosi hicho utaona huruma.
Mwendo wa Singida United hauna tofauti na timu za mitaani kwetu. Ni timu ambayo inaendeshwa kwa kudura za Mungu na haijulikani kesho yake itakuwaje.
Kawaida unapoona timu imefikia hivyo, badala ya kuendeshwa kwa mipango na mipangilio sahihi, inaanza kutegemea majaaliwa, basi jua kuna tatizo kubwa na mwisho wake huwa ni kuanguka.
Shida ninayoiona ni kwamba msimu ujao Singida United itakuwa daraja la kwanza, baada ya msimu huo, ule unaofuata itakuwa daraja la pili na hakutakuwa na nafasi tena ya kusikika kwa timu hiyo kwa kuwa safari ya kudidimia itakuwa ni ya kiwango cha lami.
Kwa nini itakuwa hivyo? Siku chache zilizopita niliwahi kuandika na kuelezea namna ambavyo Singida United ilikuwa ikionekana, timu ya Wanasiasa, maisha yake yalikuwa ni kisiasa na mwendo ulionyesha wazi hakuna mipango ya muda mrefu.
Wanasiasa wengi mipango yao ni ya leo, kesho hawataki kuijadili kwa kuwa mengi wanayofanya ni unafiki na hawana uhakika wa kuingia kesho wakiwa bado katika sehemu waliyopo.
Hivyo wanaangalia leo, wanajali watatoka vipi hapa na kikubwa inakuwa ni kuangalia uhai na hali zao na si kitu au chombo wanachokiongoza.
Nilielezea hili na ninasisitiza, kuifanya Singida United timu ya wabunge pekee au viongozi wa Simba, huku wananchi wakiaminishwa wanasiasa hao wanaoongozwa na Mwigulu Nchemba wanaweza kila kitu ilikuwa ni jambo baya sana.
Ikitokea Wanasiasa kama kawaida yao wamekimbia, wakabaki wachache mfano wa Mwigulu mwenyewe na inawezekana hawako vizuri, tatizo lao linakuwa la timu.
Kingine kibaya zaidi ni yale makosa waliyowahi kuyafanya Toto Afrika, African Sports na wao Singida United wakaingia huko kupitia Mwigulu.
Singida United ni timu inayojitegemea, timu yenye watu wake lakini Mwigulu akaifanya kuwa tawi la Yanga. Timu yenye uchungu zaidi na Yanga hata kuliko timu yenyewe.
Ilianza kudidimia African Sports, Yanga ilikuwepo na haikuwahi kutoa msaada kuikomboa. Leo imebaki kwenye historia na si timu kubwa kama ilivyokuwa ikijulikana.
Ikafuatia Toto Afrika ya Mwanza, ikawa na mapenzi makubwa na Yanga hata kuliko yenyewe. Leo inasumbuka kupambana kutoka daraja la pili na hakuna msaada wowote kutoka Yanga.
Kumbuka wakazi wa Singida, Mwanza na Tanga ni mashabiki wa Yanga na Simba. Wanaweza kuwa Singida na Yanga au Singida na Simba.
Mwigulu aligawa wachezaji wa Singida kwenda Yanga na akatangaza, akionyesha wazi anataka kuisaidia Yanga kwa kuwa hakuna wa kumzuia Singida. Wale ambao wanaipenda Simba kutoka Singida hawawezi kuiona hiyo ni timu yao na wale wa Yanga, pia hawawezi kuipenda Singida kuliko Yanga.
Mwisho ndio hiki kinaikuta Singida United leo, imekuwa timu ambayo watu wanajipigia tu, wachezaji hawajalipwa, wanakaa sehemu mbaya si za kiwango cha timu ya Ligi Kuu Bara na ile heshima yake ya misimu miwili iliyopita, imepotea kwa asilimia 90.
Singida United itateremka kwa aibu, itateremka ikiwa yatima lakini yote haya ni makosa ya siasa ndani ya soka na kujipendekeza kwa klabu nyingine wakati hiyo ni klabu inayojitegemea.
Hamkuona kwa timu zilizopita, sasa Singida United nayo imedondoka na watu wanajipigia tu, vizuri tusirudie tena.