MSIMU wa 2019/20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara taratibu unazidi kumeguka ikiwa kwa sasa timu nyingi zimebakiwa na mechi 10 na nyingine mechi 11 ili kukamilisha mzunguko wa pili.
Tunaona kwamba kwa sasa ligi imesimamishwa kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kupambana na virusi vya ugonjwa wa Corona katika hili tahadhari lazima ichukuliwe.
Ushindani unaonekana dhahiri kwa kila timu kufanya yake inapopata nafasi ya kucheza na kufanya kile ambacho wameelekezwa ili kupata pointi tatu muhimu jambo ambalo mashabiki wamekuwa wakilishuhudia ndani ya uwanja.
Kwa sasa tunaelekea lala salama, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halipaswi kulala wala kuzembea pamoja na timu zenyewe kutunza nidhamu kwa kufuata taratibu za mpira.
Licha ya kwamba kwa sasa ligi imesimama bado kuna timu ambazo zimekuwa zikipata matokeo mabovu kweye mechi zao ambazo walicheza.
Kila timu ishajua hatma yake kutokana na kutambua nini imevuna na inahitaji kufanya nini kwa kuwa imeshapata picha ya kile kinachokuja mbele yake.
Zipo ambazo zinaona kabisa nafasi yao ya kubaki ndani ya ligi ni lazima washinde mechi zote zilizobaki huku mambo yakiwa magumu hakuna namna ni lazima wapamabane kushinda mechi zao.
Moto kwa waamuzi ambao wanafanya uzembe kwa makusudi uendelee usipoe pia elimu wapewe kwa kuwa nao ni binadamu wanapaswa wakumbushwe namna ya kufanya ili wafuate sheria 17.
Waamuzi wanashikilia furaha na maumivu ya timu iwapo watashinwa kutenda haki kinachotakiwa ni kuwa katika maadili na kufuata kanuni hakuna jambo lingine linalotakiwa kwa sasa zaidi ya utekelezaji.
Kwa wale viongozi ambao wanashindwa kuheshimu miiko ya kazi wanapaswa wachukuliwe adhabu ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanafanya makusudi kutimiza wajibu wao.
Kwenye utendaji wa kazi ni muhimu kuongeza umakini na kuacha dharau kwani haijengi na sio utamuduni kwenye ulimwengu wa michezo.
Waamuzi walikuwa wanafanya maamuzi yao kwa kuwa hakuna aliyekuwa anawafuatilia na hata kama wanafuatilia basi walikuwa wanachelewa kutoa maamuzi hali iliyokuwa inaongeza kiburi.
Timu nyingi zinacheza mechi ambazo hazirushwi na Azam TV ni mbaya kutokana na rekodi zao kuwa mbaya pindi wanapochezesha mechi za aina hii na ushahidi kukosekana hasa kwa wale ambao wataamua kutoa malalamiko yao.
Rai yangu kwa TFF kuwa macho muda wote kwenye mechi hizi ambazo kila mmoja anapigania timu yake ipate matokeo bila kujali anacheza na nani na katika wakati gani hilo hajui zaidi ya kutazama matokeo chanya kwake.
Mechi za ugenini kwa sasa zinakuwa ngumu kwa timu zote kutokana na kuwepo kwa kampeni ya kila timu ishinde mechi zake za nyumbani hili ni gumu na baya kwenye soka letu kwani halileti ushindani bali linazalisha chuki.
Hakuna ambaye anapenda kupata matokeo mabaya kwenye michezo yake ya mwisho hali inayofanya wengi kulazimisha mambo ambayo wanayatarajia kutokea hili halijakaa sawa.
Kwa mechi ambazo ni za lala salama na hazitapata nafasi ya kuonyeshwa na Azam TV kuna umuhimu wa kuwa katika uangalizi maalumu ili kupunguza janjajanja za kampeni ya kila mmoja ashinde mechi zake.
Ili kuepukana na maamuzi haya TFF ni lazima iwafuatilie waamuzi kwa ukaribu hatua kwa hatua na kutoa maamuzi hapohapo na sio kuwafungia macho wanaua soka letu kwa mapenzi yao binafsi.
Sheria 17 lazima zifuatiliwe na viongozi wa timu wanapaswa wakomae kwenye maandalizi na sio kutaka kushinda nje ya uwanja hili halipo sawa ndio maana tunapata timu ambazo zinashindwa kufika mbali.
Ukubwa wa Ligi Kuu Bara unatakiwa uthaminiwe na kila mmoja ambaye ana timu bila kujali aina ya timu aliyonayo na ile ambayo anacheza nayo itakuwa ajabu kupata matokeo ya mezani.
Naona kuna timu ambazo zinajitetea kushuka daraja ila zinatakiwa zitumie mbinu bora ya kushinda mechi na sio kutengeneza hujuma kwa kanda ama mikoa ambayo ina timu ambazo hali yake sio nzuri.
Kila mkoa kwa sasa naona kumekuwa na kampeni ya kutaka kuona timu zao zinashinda michezo yao yote hii ni mbaya na inaua ushindani waziwazi waache timu zishinde kwa kupambana.
Kama kuna timu ambayo inapanga matokeo kwa njia zake za ujanjaujanja ikikibainika inatakiwa ichukuliwe adhabu kali na iwe mfano kwa timu nyingine zenye tabia kama hiyo ziache mara moja.
Tunataka bingwa apatikane kwa uhalali na sio kuungaunga mpaka apatikane italeta dosari kwenye soka letu hasa wakati wa mashindano ya kimataifa.
Ligi Kuu Daraja la Kwanza pia ni muhimu kuongeza umakini kwani tayari timu zimeanza kujijengea ufalme wao kwamba lazima zipande na kushiriki kwenye ligi.
Zipo zile ambazo zimeona mwanga wa kushiriki moja kwa moja kwenye ligi na nyingine zinatambua kwamba zitaangukia kucheza play off hizo nazo zimeanza kufanya madudu yao ili wakutane na timu ambazo wanazitaka.
Katika hili kwa timu ambazo zinapambana kupanda daraja zinatakiwa zikumbuke kwamba atakayepanda kwa hila atashuka bila kutarajia kwani kupanda ni habari nyingine na kushinda mikikimikiki ni habari nyingine.