NYANDA za Kanda za Juu Kusini kuna timu mbili ambazo zinapambana ndani ya Ligi Kuu Bara zikiwa kwenye mipango tofauti kwa sasa.
Namungo ya Ruangwa ipo mkoani Lindi Uwanja wake ni Majaliwa ambao ni sehemu yao ya kutambia wakiwa nyumbani na wakisepa ugenini bado wamekuwa wakionyesha cheche zao.
Timu nyingine ni ya Mtwara hapa unakutana na Ndanda FC wao Uwanja wao ni Nangwanda Sijaona hawa nao kama sijawaelewa vizuri namna wanavyokwenda ni sawa na Singida United hivi.
Ngoja kabla hatujafika mbali tuigusie kidogo Namungo ambayo imetoka kumalizana na Yanga Machi 15 Uwanja wao wa Majaliwa na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1.
Kwa namna ambavyo kasi yao inakwenda inafurahisha kwa kuwa ni mwanzo na inahuzunisha hasa wakati ujao endapo itayumba na kufikia kama hali ya Singida United.
Timu inaonekana inashindana na inapata matokeo kwa sasa na kumekuwa na kelele nyuma ya pazia kwamba hii timu inabebwa kutokana na kuwa na mkono wa wanasiasa ndani ya klabu hiyo.
Sina uhakika na kelele hizo kutokana na kuwaona wakiwa uwanjani wanacheza na juhudi zinaonekana kwa sasa labda moto wao umepanda kutokana na kuona kwamba ni mwanzo wa ligi baadaye watapoteana itakuwa sio sawa.
Itapendeza kasi ambayo wapo nayo kwa sasa wakaendelea kwenda nayo hata msimu ujao kwani kwa sasa tupo kwenye lala salama kutokana na ligi kuanza kufika ukingoni.
Narudi sasa kwa ndugu zangu wa Mtwara hawa Ndanda wanakuchele hapa kuna shida ambayo ipo na inaendelea kuendelea kuwa ndani ya timu kwa sasa.
Tumeona mwanzo walianza kwa kusuasua na walishindwa kufurukuta kwenye mechi zao za mwanzo na hakuna ambaye alikuwa akiwatazama wala kuwapa sapoti.
Ninaona kwamba kwa sasa watu wa Mtwara wamezinduka na kuanza kuipa sapoti timu yao ili kuona inabaki ndani ya ligi tena msimu ujao.
Hili ni balaa kwa watu wa Mtwara ambao wanakuja kukumbuka shuka kukiwa kumepambazuka juhudi zilitakiwa zianze kuonekana mwanzo wa ligi jambo litakalofanya ushindani kuwa mkubwa.
Uzuri ni kwamba mchezo wa soka ni kitu ambacho hauwezi kukificha kwani kila mmoja anaona ndivyo ilivyo kwa sasa kwa wachezaji na mashabiki.
Ndanda inaanza kujinasua taratibu kutoka kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja na imeanza ikiwa imepoteza kwenye mechi zake zilizopita jambo ambalo linawafanya kwa sasa watumie nguvu kubwa.
Ukitazama msimamo kwa sasa ipo nafasi ya 16 baada ya kucheza mechi 29 kibindoni ina pointi 31 ilizojikusanyia kwenye mechi zake ilizocheza.
Imenyooshwa kwenye mechi 12 sare 10 na imeshinda mechi saba kwenye mechi zake ilizocheza mpaka leo jambo ambalo bado ni gumu kwake kuibuka ndani ya 10 bora.
Ikiwa na mechi tisa mkononi ina kazi ya kupambana ili isishuke daraja kwani bado haipo sehemu salama kwa sasa licha ya kuwa ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo.
Msimu huu timu nne zinashuka jumla na kwanafasi ambayo ipo ni maalumu kwa ajili ya kucheza playoff hivyo kama itamaliza ligi ikiwa hapo ilipo itaishia kucheza playoff ili kutetea nafasi yake ya kubaki ndani ya ligi.
Kwangu mimi naona wakati uliopo kwa mashabiki wa timu zote Bongo wanapaswa wajifunze kuzipenda timu zao tangu awali na sio kusubiri kipindi kigumu ndio wanaanza kuipa sapoti timu yao.
Ugumu uliopo kwa sasa timu ikipoteza mechi zake zinazofuata nafasi yake ya kubaki ndani ya ligi pia inakuwa ngumu wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizobaki.
Darasa la bure kwa timu ambazo zipo ndani ya 10 bora kwa sasa mashabiki wajifunze kuwa na sapoti kwa timu bila kubagua hii inaongeza nguvu kwa wachezaji kuendelea kupambana kufikia malengo waliyojiwekea.
Suala la kukurupuka kwa kuwa timu inashika nafasi ya mwisho na kuanza kampeni ya kuichangia ili isishuke daraja hili ni jambo baya na la ajabu kwa ligi yetu.
Endapo timu itashuka daraja sio timu peke inayopata hasara bali hata wachezaji pamoja na timu zinakuwa kwenye wakati mgumu kwa ajili ya wageni ambao wamekuwa wakiitembelea Mtwara wakati wa mechi.
Inapaswa iwe mwanzo na mwisho kwa mashabiki wanaoacha timu inyooshwe kwanza kwenye mechi zake kisha wanakuja kuikumbuka mwishoni hali inakuwa tete.
Kila shabiki na mkazi wa Mtwara inapaswa atambue kwamba kila mmoja anapenda kuona timu inapata matokeo na kila mmoja anafanya kile ambacho kitakuwa bora kwake ndio maana hata nilipoamua kuitazama Ndanda nilichangua kutokana na mwenendo wake ulivyo.
Mashabiki wa Ndanda inabidi muelewe kwamba timu hiyo ikisepa kwenye ligi msimu huu itakaporeja kuna mambo mengi yatakuwa yamebadikika kutokana na ushindani ambao upo kwasasa.
Mpango mkubwa baada ya kusimamishwa kwa ligi kutokana na kupambana na virusi vya Corona na Ndanda kutangaza kuvunja kambi kuna umuhimu wa kuendelea kupambana ili kulinda afya zetu na Taifa kiujumla huku mbinu mpya ya ushindi ikitafutwa baada ya muda wa siku 30 kukamilika.