Home Uncategorized KESI YA POLISI, RUVU SHOOTING NI HADITHI INAYOONYESHA UTOTO

KESI YA POLISI, RUVU SHOOTING NI HADITHI INAYOONYESHA UTOTO



Na SALEH ALLY
LAZIMA utakuwa umesikia mzozo ulioibuka kati ya Polisi Tanzania dhidi ya Ruvu Shooting kila upande ukitupa lawama kwa mwingine kwamba ulikuwa chanzo cha vurugu wakati timu hizo zilipokutana mjini Moshi.
Polisi Tanzania walikuwa wenyeji na wanalalamikiwa kuwafanyia ubabe Ruvu Shooting wakati wakiingia kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Katika vurugu hizo baadhi ya maofisa wa Ruvu Shooting waliumizwa akiwemo Kocha Mkuu, Salum Mayanga ambaye inaelezwa alilazimika kutibiwa baadaye.
Polisi wao wanamtuhumu Mayanga kwa kufanya vurugu wakati timu yake ikiingia uwanjani na kusisitiza kuwa Shooting walifanya vurugu kubwa.
Uongozi wa Polisi wenyewe unaamini ulifanyiwa vurugu na Ruvu Shooting tena shutuma kubwa zinaelekezwa kwa msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire kwamba amesema uongo akisisitiza alikuwa uwanjani wakati wa vurugu hizo akielezea kilichotokea. Lakini wao wanasema hawakumuona na anazungumza uongo.
Masau anasisitiza alikuwepo, alilazimika kuingia kwenye mlango mwingine kwa uficho kutokana na kupata taarifa kwamba alikuwa amewekwa kwenye kundi la watu ambao walitakiwa kufanyiwa vurugu na Polisi.
Sasa, tayari Masau amepelekwa kwenye kamati ya nidhamu kwa tuhuma za kusema uongo na anasubiri kuhojiwa ingawa tayari yeye ameanza kuhoji akisema kamati yenyewe imemuita na kumhukumu kwa kusema alisema uongo badala ya kusema anatuhumiwa.
Ni kama hadithi fulani ya “kitoto” inavutia hivi na ungependa kuisikiliza hadi mwisho lakini kwa sasa majibu yatapatikana baada ya kamati kukaa na kutoa uamuzi kuhusiana na kilichotokea.
Uhalisia tutaujua baadaye lakini nataka nikukumbushe hizi timu zinazozana, zote ni za majeshi ambazo kwa kawaida unategemea kusikia ndio zinazoongoza kwa nidhamu kwa kuwa zina malezi ya kijeshi.
Timu za majeshi zinapaswa kuwa na nidhamu zaidi kuliko ilivyo sasa. Lakini tukubaliane kwamba kumekuwa na tabia ambazo si nzuri na za kibabe bila ya sababu kutoka kwa timu nyingi za majeshi.
Wale ambao wanakuwa nje wamekuwa wakifanya vurugu mara kadhaa na tunajua. Mfano mzuri daraja la kwanza tumeona rundo la vurugu na mara nyingi timu za majeshi zimekuwa zikihusika.
Ubabe bila sababu umekuwa ukifanywa na askari kwa waamuzi, mashabiki wa timu pinzani na wakati mwingine hata Waandishi wa Habari wakizuiwa kufanya kazi zao vizuri kibabe tu.
Kawaida unawaona wanaofanya vurugu hizo wanakuwa wakifanya hivyo si kwa niaba ya jeshi lao lakini wanafanya hivyo wakijua wako salama na hakuna wa kuwachukulia hatua, hili si jambo sahihi.
Mara kadhaa, tumeona picha za video waandishi wakinyanyaswa kwa visingizio mbalimbali. Kama wakijaribu kujikomboa kunakuwa na kisingizio kuwazuia askari wasifanye kazi yao. Wako wamewekwa mahabusu bila sababu basi ili mradi tu.
Najua mnaweza mkaniuliza maswali mengi lakini mimi niwe mtu ambaye ningependa kuwaambia moja kwa moja bila ya woga. Mnapaswa kufuata taratibu zinavyotaka, na vizuri mkawa mfano wa kuigwa kwa kuwa sifa ya majeshi ni nidhamu.
Inawezekana majeshi hayana nia ya vurugu au kuvuruga nidhamu. Lakini waliomo wakaitumia nafasi ya ukubwa na heshima yake vibaya kwa kufanya mambo hayo yasiyo na tija wala msaada wowote.
Hili la nyie wenyewe kushitakiana, hakuna ushahidi, kila mmoja analia kuwa yeye ndiye kakosewa na malalamiko yanayoashiria kuna ‘utoto’ ndani yake, yanaweka wazi kuwa ndani yenu mna walakini.
Inawezekana ingekuwa timu ya kiraia leo ingekuwa kimya. Lakini kwa kuwa vyuma vilikutana hakuna aliyekubali kushuka, mkapambana. Nafikiri wakati huu uwe sehemu ya funzo kwenu na itakuwa vizuri mkabadilika kuliko kuendelea kukosea halafu mkaendelea kusema hamkufanya na wanaosema kuwaona wabaya mkitaka kuwatisha tena. Huu ni mpira, mmeamua kuwa huku, chezeni mpira na si vimbwanga.

SOMA NA HII  MANCHESTER CITY YAFUNGIWA MIAKA MIWILI KUSHIRIKI LIGI YA MABINGWA ULAYA