WAKALA Kassa Mussa ambaye anamuwakilisha beki kisiki anayekipiga kwenye timu ya Coastal Union, Bakari Nondo Mwamnyeto amekanusha uvumi unaoendelea kuhusu mchezaji wake kuhusishwa na kujiunga na timu ya Simba.
Ambapo amezionya timu zitakazojaribu kufanya makubaliano na mchezaji wake kinyume na utaratibu,atazichukulia hatua za kisheria.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa Simba inajiandaa kutoa Sh miliini 85 pamoja na gari ili kufanikisha dili la kumsajili mchezaji huyo.
Akizungumzia ishu hiyo, Kassa ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1988, amefunguka kuwa timu za Simba na Yanga zimewahi kumtafuta kuhusiana na kutaka huduma ya mchezaji wake lakini hawakufi kia makubaliano yoyote.
“Bakari hajafanya makubaliano na timu yoyote na kinachoendelea ni uvumi, kuna timu iliwahi kunitafuta na kutaka kutoa fedha za awali lakini nilipinga suala hilo, na mimi siwezi kufanya kitu chochote bila kuhakikisha kwanza timu inayomtaka Bakari inamalizana kwanza na Coastal Union ambao ndiyo wamiliki halali wa mchezaji huyo kwa sasa,” alisema Kassa.
Mwamnyeto amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu akiisaidia Coastal Union kushika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, pia amekuwa mmoja wa mabeki muhimu wa timu ya taifa ya Tanzania.
Wakati huohuo, alipotafutwa Mwamnyeto mwenyewe alisema: “Kazi ya mchezaji ni kucheza mpira popote pale, kwa sasa ninawasubiri Simba ili nimalizane nao nikakipige kwao, sina mashaka na uwezo wangu na kila kitu kinawezekana.”