ZIMEBAKI saa zisizozidi 72 kabla ya kumalizika kwa siku 30 za kusimamishwa shughuli zinazohusu mikusanyiko zilizotangazwa na serikali katika kukabiliana na janga na ugonjwa wa covid-19, huku mashabiki wa soka na burudani wakisikilizia kuona mambo yatakuwaje baada ya kukosa uhondo kwa muda wote huo.
Serikali ilizuia shughuli zenye mikusanyiko na kusababisha kusimamishwa kwa Ligi na michezo mingine sambamba na burudani, lakini bado Mwanaspoti limekuwa likiwapa uhondo kupitia kona hii ya Tujikumbushe inayorejea baadhi ya matukio ya michezo yaliyojiri miaka iliyopita.
Leo katika fukuafukua tumejikuta tukirejea hadi mwaka 2011, tarehe kama ya leo, Aprili 13, nyota wa Simba, Emmanuel Okwi aliwaomba radhi wanachama na mashabiki wa Simba kwa kitendo cha kukosa penalti kwenye mechi yao ya mwisho ya msimu wa 2010-2011 dhidi ya Majimaji.
Okwi alikosa penalti baada ya mkwaju wake kugonga mlingoti na kuikosesha timu yake kutetea ubingwa mbele ya watani wao waliopoka kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mchezo huo uliopigwa jijini Dar es Salaam Simba licha ya kushinda mabao 4-1 dhidi ya Majimaji na kuishusha daraja, iliishia kulitema taji kwa Vijana wa Jangwani, waliomaliza msimu kwa kuifumua Toto Africans kwa mabao 3-0 jijini Mwanza.
Ushindi huo uliifanya Simba kukaa kileleni kwa kuwa na mabao mawili zaidi ya watani wao, licha ya kila moja kumaliza msimu na pointi 49 baada ya kila timu kucheza mechi 22.
Simba ilifunga mabao 40 na kuruhusu 17 na kuwa na tofauti na mabao 23, wakati watani zao wakimaliza na mabao 32 na kufungwa saba tu na hivyo kuwa na ziada ya mabao 25, hivyo Okwi aliamini kama angefunga penalti ile ingewaongezea morali wa kupata mabao mengine zaidi.
Okwi alisema anajisikia vibaya kwa kushindwa kufunga bao ambalo lingewapa nafuu Simba katika kutetea ubingwa dhidi ya watani wao waliowanyang’anya ubingwa wao waliotwaa msimu wa 2009-2010 bila kupoteza mechi hata moja.
“Niwaombe radhi mashabiki wa Simba kwa kukosa penalti dhidi ya Majimaji kwani naamini tulikuwa na nafasi ya kutetea ubingwa, lakini wakati mwingine soka ndivyo lilivyo na yeyote anaweza kukosa penalti. Narudia kuwaomba radhi,” alinukuliwa Okwi huku akidai wanaenda kujipanga kwa msimu ujao akiamini watarejesha ubingwa Msimbazi.
Kauli hiyo ya Okwi ilitokea kweli kwani msimu wa 2011-2012 alisaidiana na wenzake kuibeba Simba na kurejesha taji Msimbazi, huku wakiifumua Yanga mabao 5-0 katika mechi yao ya kufungia msimu ulitumika pia kukabidhiwa kombe lao walilonyang’anywa.