LUIS Miquissone nyota wa Simba amejikuta kwenye wakati mgumu kufuatia baadhi ya watu ‘matapeli’ kutumia jina lake katika mitandao ya kijamii kuomba pesa kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo.
Kiungo huyo alimejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa imemtoa kwa mkopo katika klabu ya UD do Songo kutoka kwao Msumbuji.
Luis ametoa malalamiko hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa kuna baadhi watu wamekuwa wakitumia jina lake katika mtandao huo na kufanya kazi ya kuomba pesa kutoka kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo kitu ambacho siyo sawa kwa upande wake.
Mchezaji huyo ambaye kwa sasa yupo kwao nchini Msumbiji kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosambazwa na virusi vya Corona aliandika: “Nasikitika kuwaambia kuwa kuna mtu amefungua akaunti yenye jina langu na anaposti kila kitu ninachoposti kwa muda mrefu sasa.
Kama hiyo haitoshi, ameanza kuwa-DM (kutuma meseji za siri) mabosi na wachezaji wenzangu akiwaomba pesa.
“Nitaripoti suala hili katika mamlaka husika na wakati huohuo tafadhali naomba mnisaidie kusambaza ujumbe huu pamoja na ku-unfollow akaunti hiyo ambayo siyo sahihi,” ilisomeka taarifa hiyo.