KIUNGO mzawa anayekipiga ndani ya Yanga, Mrisho Ngasa amesema kuwa bado anavuta pumzi ya kurejea Dar es Salaam rasmi akiendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
Wakati Ligi Kuu Bara inasimamishwa na Serikali, Machi 17 kabla ya Aprili 14 taarifa kutolewa kwamba bado ligi itasimamishwa Ngasa alikuwa zake Mwanza na amerejea hivi karibuni na kujichimbia Bagamoyo.
Ngasa amesema kuwa ameweka makazi yake Bagamoyo huku akifanya mazoezi mepisi kulinda kipaji chake na kumshangaa mchezaji mwenzake Deus Kaseke ambaye kwa sasa yupo Mbeya.
“Nipo Bagamoyo kwa sasa nimetulia sehemu nzuri nafanya mazoezi ili kulinda kipaji changu nikimaliza ninapata muda wa kupumzika pia.
“Namshangaa Kaseke yeye yupo Mbeya muda wote hajawahi kutoka Mbeya hajui tu kwamba akiwa huko hajifunzi jambo, na mtindo wake wa kutupia video kwenye mitandao watu watamuibia mbinu,” amesema.