AZAM FC mabosi wao bado wanakuna kichwa juu ya maisha yatakuaje mara baada ya wachezaji wao kurejea kama hali ya ugonjwa wa corona itatulia.
Mtendaji Mkuu wa Azam Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema bado wanasikiliza maelekezo ya Serikali juu ya kutulia kwa maambukizi ya corona ambayo yatatoa picha ya lini kikosi chao kitarejea kazini.
Popat amesema endapo hali itatulia kisha wachezaji wao kurejea waliokwenda makwao watakuwa na tahadhari kubwa katika kambi yao.
Bosi huyo amesema kikosi chao kikubwa ndio kitatangulia kurejea kazini kutokana na majukumu yake ambapo kila mchezaji atatumia chumba chake.
Amesema wameamua kufuta kwa muda wachezaji kulala wawili wawili licha ya kwamba kila mmoja hutumia kitanda chake kwa lengo la kuwaangalia vyema kukwepa maambukizi.
Amesema vikosi vya timu za vijana wao watasubiri kidogo kuangalia mwenendo wa timu yao kubwa kisha nao watarejea baadaye endapo watajiridhisha hali iko salama.
Aidha Popat amesema kwasasa wameendelea kuwa karibu na mawasiliano na wachezaji wao waliorudi makwao ndani na nje ya nchi kufuatilia hali zao na hata jinsi wanavyotekeleza ratiba ya mazoezi ambayo waliachiwa na kocha wao Aristica Cioaba.