ALIYEKUWA kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amemwambia, straika nguli wa Simba, John Bocco, 30, bado anaweza kutisha katika soka la Afrika nje ya Tanzania licha ya umri kumtupa mkono.
Zahera alisema Bocco, ambaye Agosti 5 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 31, ni kati ya wachezaji ambao alikuwa anawakubali katika ligi ya Tanzania na alikuwa anamuwazia awe na mtazamo wa kusaka fursa nje.
Alisema anaamini Bocco ana uwezo wa kucheza nchi yoyote ya Afrika endapo akiamua kuifikirisha akili yake na kusaka fursa mpya.
“Anajua kujiweka katika eneo la kufunga, ana uwezo wa kufunga kwa kuchwa na miguu, umbo lake linambeba kuwa na sifa za ushambuliaji,”
“Ana heshima yake Ligi Kuu Bara, asikubali akamaliza soka kwa kuishia kucheza Tanzania na naona amechelewa kutoka angefanya hivyo mapema asingejutia kwani naamini angefanya makubwa,” alisema kocha huyo ambaye bado hajasaini dili mpya baada ya kutoka Yanga.
Alisema kwa namna alivyoona vipaji Tanzania endapo wachezaji wakaamua kujitoa asilimia 100 basi wengi wataweza kupata nafasi ya kufanya vyema nje.
Zahera alisema amemfundisha pia kiungo wa Yanga, Mapinduzi Balama alimuona anastahili kucheza soka nje, akimsisitiza asichelewe kufanya uamuzi.
“Anapoamua kwenda kucheza nje anakuwa anafikiria faida zake binafsi na timu yake ya Taifa kupata changamoto mpya atakazokuwa anakumbana nazo huko,
“Atakutana na mifumo tofauti, wachezaji tofauti na mbinu tofauti hata kifikra atabadilika na kuwa mtu wa kuwaza makubwa zaidi hivyo namshauri awe na mawazo mapema,” aliongeza Zahera ambaye aliukana uraia wa DR Congo na sasa ni Mfaransa anaishi sehemu moja na Nicolas Anelka.