Home Uncategorized CHAMA ATIBUA DILI LA MKUDE, NDEMLA YANGA

CHAMA ATIBUA DILI LA MKUDE, NDEMLA YANGA

WACHEZAJI wawili ndani ya kikosi cha mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara Simba ambao wote ni viungo, Jonas Mkude na Said Ndemla, watakuwa wamepoteza dili lao Yanga kufuatia sakata la hivi karibuni lililomuhusisha Mzambia Clatous Chama ikidaiwa kufanya mazungumzo na kiongozi wa Wanajangwani.

Hivi karibuni ilitokea msuguano kati ya uongozi wa timu hizo mbili, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, kudai alifanya mazungumzo na mchezaji wa Simba ili asajiliwe katika klabu yake na baadaye akaomba radhi na kudai kwamba ilikuwa ni utani.

Habari ambazo gazeti la  DIMBA limezipata kutoka ndani ya klabu hiyo, zimesema kwamba kabla ya Mwakalebela kumtaja Chama, wachezaji waliokuwa wanafikiriwa na Yanga ni Mkude na Ndemla, lakini kutokana na migongano hiyo kwasasa wamenyoosha mikono.

Kiongozi mmoja mwandamizi aliliambia gazeti la  DIMBA kwamba, mara nyingi usajili unaofanywa na timu hizi mbili umekuwa ukiendeshwa kwa siri lakini kutokana na hali ilivyo kwasasa si rahisi kufanikisha mpango wa Ndemla na Mkude.

“Kama kuwaliza Simba ingekuwa ni kwa Mkude na Ndemla, hawa tulitaka tuwasajili kwa pamoja na kuwatambulisha siku moja, lakini sasa Simba watakuwa makini nasi tumeachana na wachezaji wao,” alisema.

Awali ilidaiwa kwamba Mkude ambaye amewahi kutajwa sana akihusishwa kwenda Yanga na Ndemla ambaye msimu uliopita alitajwa kutakiwa na mabingwa hao wa zamani, wangetinga Jangwani msimu ujao kama mambo yangekwenda sawa.

Hata hivyo ujio wa Mkude ndani ya kikosi cha Yanga huenda ungekutana na vikwazo kutokana na nyota huyo kuwa kipenzi cha mwekezaji mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kuhusu Ndemla ambaye pia ni miongoni mwa wachezaji waliodumu muda mrefu katika kikosi cha Simba na mwenye maelewano mazuri na Mo, safari yake ingekuwa rahisi kutokana na Yanga kumuahidi kumpa nafasi kubwa ya kucheza tofauti na Msimbazi ambako mara nyingi amekuwa akianzia benchi.

SOMA NA HII  DAU LA BEKI ANAYEWINDWA NA SIMBA NI PASUA KICHWA