Home Uncategorized KUNA UMUHIMU WA KUWAPA THAMANI WACHEZAJI WETU ILI KUWA BORA, MWAMNYETO NI...

KUNA UMUHIMU WA KUWAPA THAMANI WACHEZAJI WETU ILI KUWA BORA, MWAMNYETO NI WAKATI WAKE

KILA mtu anajukumu la kuongeza thamani ya maisha yake, ukiwa ni mtu wa kwenda kulala kwenye gesti za elfu saba, kila mtu ataona thamani yako ni elfu saba!
 Ukiwa ni mtu wa kusafiri kwa ndege, hakuna atakayehitaji kukuletea tiketi ya basi! Tanzania kuna malalamiko mengi sana juu ya thamani za wachezaji wa kigeni kuwa juu kuliko wachezaji wazawa, Unadhani imekuja kwa bahati mbaya? Hapana. 
 Wachezaji wa Kigeni wengi wanajitambua na wamekuwa wajanja kwa kutumia watu kuongeza thamani zao, moja kati ya timu zilizokuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu Bara ya msimu huu ni pamoja na Coastal Union ya mkoani Tanga ambako ndani yake yupo mmoja wa walinzi bora wa kati kwa sasa nchini, Bakari Mwamnyeto.
Huyu ni mwamba hasa, anajua kucheza vizuri mipira ya juu, anajua vizuri kutumia miguu yote, ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira na pia, mjuzi wa kuanzisha mipira mirefu, huyu jamaa ni VVD wa Coastal Union. 
Nani anamuongezea thamani Bakari Mwamnyeto? Hakuna jibu, kuna uwezekano hata ukienda klabuni kwake hakuna anayejua hata idadi ya mechi tu alizocheza tangu ajiunge hapo, Huenda hakuna anayejua idadi ya dakika alizocheza msimu huu katika hali hii kumuongezea thamani haiwezi kuwa jambo rahisi.
Mwamnyeto ndiye mwamba imara pale kwa Wagosi wa Kaya, kimo chake ni biashara tosha, Umri wake ni sifa nyingine ya ziada. Kuna kitu tunapaswa kukiongeza kwa wachezaji wetu badala ya kulalamika lazima tujifunze kwa watu waliofanikiwa. 
Harry Maguire wakati yuko Leicester City pengine alikuwa ni beki tu wa kawaida lakini wakati wanataka kumuuza kwenda Manchester United, thamani iliongezeka na bei ikapanda.

 Stori ni ileile kama ilivyokuwa kwa Virgil van Dijk wakati anakwenda Liverpool. Maisha yake ndani ya Southampton yalikuwa ya kawaida sana lakini wakati anakwenda Liverpool, hali ilibadilika na maisha yaligeuka.
  Tunakwama wapi? Usinipe jibu, Mwamnyeto kila timu kubwa ya nchi hii inamtaka Simba na Yanga wote wanamtolea macho, alihitaji kupata mtu makini sana wa kumsimamia.
 Anahitaji kuwa na mtu mwenye taaluma ya kuongeza thamani yake, Anahitaji kuwa na mtu wa kumfanyia promosheni. Ni mchezaji mzuri sana lakini anaweza kuuzwa bei ya mbuzi tu.
 Wachezaji wetu kama kuna kosa kubwa wanalofanya ni kwenda mezani kujadili maslahi yao wenyewe, kama kuna kitu wanakosea ni kusaini mikataba bila kuwa na mwanasheria. Mchezaji wa mpira anaongezewa thamani hapo.
 Kila mahali wanafanya hivyo lakini hapa kwetu watu wanalalamika tu! Mitandao ya kijamii ina nguvu kwenye dunia ya leo, lakini wangapi mnafahamu hata jina la akaunti yake? Usinipe jibu. Kupitia mtandao wa YouTube kumekuwa na matukio mengi, yanayotazamwa huko, umewahi kujua akaunti ya Bakari Mwamnyeto? Usinipe jibu.
 Haya siyo mambo ya kumlaumu, anahitaji watu walioko nyuma kumsaidia. Siyo tatizo la mchezaji husika ni tatizo la mfumo wetu wote wa mpira, ni jukumu la kila mmoja wetu kuongeza thamani ya maisha yake, kama Coastal Union wanataka kumuuza Mwamnyeto kwa bei kubwa ni lazima wamuongezee thamani.
 Ni Bonge moja la mchezaji, ni fundi kwelikweli na ana umri mdogo. Ni lazima azungumzwe sana na vyombo vya habari, ni lazima atafutiwe wadhamini, hii siyo shughuli ndogo, inahitaji watalaamu nyuma yake.
 Ungemuuza bei gani Bakari Mwamnyeto? Nasubiri maoni yako kwenye namba yangu ya simu hapo juu. Ni kawaida mchezaji aina ya Bakari Mwamnyeto kuwa na mkataba wa mwaka mmoja tu pale Coastal Union. Wachezaji wetu wanapewa mikataba ya muda mfupi hata kama wana uwezo mkubwa.
 Kuna sababu za umasikini wa fedha na kuna sababu za umasikini wa fikra, kuwa mchezaji bora ni jambo moja na kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa ni jambo la pili.
 Hilo la kwanza linahitaji zaidi kipaji cha mchezaji na juhudi zake lakini, hilo lingine ni jambo la kitaalamu, linahitaji watu wenye uelewa mpana kwenye biashara ya soka.
SOMA NA HII  RASTA KUTOKA BURKINA FASO KUTUA YANGA,SIMBA DAKIKA 270 BINGWA,NDANI YA CHAMPIONI JUMAMOSI