Home Uncategorized VIGOGO YANGA WAMGEUKA EYMAEL KUHUSU YONDANI KUTUPIWA VIRAGO

VIGOGO YANGA WAMGEUKA EYMAEL KUHUSU YONDANI KUTUPIWA VIRAGO

YANGA wameperuzi ripoti ya mapendekezo ya Kocha wao Luc Eymael wee lakini walipofika kwenye jina la Kelvin Yondani wakaganda kidogo. Wakakubaliana kutokubaliana.

Ripoti ya siri ya mipango ya Kocha Eymael kwa uongozi imemtaja Yondani kama itawezekana kumpata beki mwingine mzawa mwenye ubora zaidi basi aletwe na mkongwe huyo aonyeshwe mlango wa kutokea.

Mabosi wa Yanga bado wanaona Yondani sio silaha ambayo inatakiwa kuachwa kwa sasa ni kama watakuwa wanashindwa kuheshimu wachezaji wakongwe na wamenusa Simba na Azam wakaona kuna uhitaji wa Yondani na wanaeza kuwa wanawauzia adui silaha ingawa mwishowe wanakubaliana Luc ndiye Kocha.

“Kumuacha Yondani sasa ni kama kuuza silaha kwa adui yako, sawa tunajua mapungufu yake lakini sio afya kumwacha kwa sasa,” alifunguka bosi mmoja ambaye yuko katika kamati ndogo ya usajili wa timu hiyo.

“Tunajua sio beki anayeweza kwenda kucheza muda mrefu lakini ukongwe wake ni silaha hilo hatutaki lije lituletee shida,” aliongeza kiongozi huyo na kusisitiza walichokubaliana watamshawishi Kocha aongezewe mkataba wa mwaka mmoja kuangalia mwenendo wake.

Mkataba wa Yondani unamalizika mwisho wa msimu huu na mwenyewe anajua ndani ya klabu kuna sintofahamu ya kama ataendelea kusalia hapo au vinginevyo na hivi karibuni Mwanaspoti linafahamu beki huyo alishawapa mkono wa kwaheri baadhi ya marafiki zake ndani ya timu kwa kuwaambia hana hakika ya kuwemo msimu ujao.

Mmoja wa wachezaji wa Yanga aliiambia Mwanaspoti Yondani amemhakikishia anarudi nyumbani (Simba) kumalizia maisha yake ya soka na anaamini atacheza kwa nguvu zote kutokana na aina ya timu waliyonayo kwa sasa.

Mbali na maamuzi hayo vigogo hao ambao wanafanya kazi kwa ukaribu na wadhamini wao GSM katika kukamilisha usajili mpya, pia wamekubaliana atafutwe beki wa kati wa nguvu ndani na nje atakayekuja kumpa changamoto Yondani na hata mabeki wengine ndani ya kikosi hicho.

Ingawa Yondani mwenyewe imekuwa ngumu kusikia kutoka kwake, lakini Eymael aliiambia Mwanaspoti kwa sasa hawezi kutaja majina ya nani anaachwa au anabaki bali ana mipango yake na amewasisitiza viongozi kuwaongezea wale muhimu mikataba mipya.

SOMA NA HII  RATIBA YA LIGI KUU BARA LEO OKTOBA 22, YANGA NA SIMBA KAZINI

Lakini Kocha huyo akasisitiza katika mipango yake ya kuongeza wachezaji wapya eneo la ulinzi ataligusa ili kuongezea changamoto waliopo wapandishe zaidi viwango vyao.

Hii inakuwa mara ya pili kwa mabosi wa klabu hiyo kuzuia jaribio la kumwacha Yondani kwani enzi za kocha Hans Pluijm aliwahi kumtaja beki huyo katika ya anaotaka kuwaacha na mabosi wa klabu hiyo kuzuia wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati ya mashindano wakati huo Mhandisi Issac Chanji.