KUREJEA kutoka kwenye majeraha kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman ‘Sheva’ kumezuia usajili wa kiungo wa Polisi Tanzania, Sixtus Sabilo na Lucas Kikoti anayekipiga Namungo FC.
Kikoti na Sabilo ni kati wa viungo washambuliaji wanaotajwa kutakiwa na Simba kwenye msimu ujao katika kuiboresha safu ya kiungo ya timu hiyo.
Simba chini ya mwekezaji wake bilionea, Mohammed Dewji, imepanga kufanya usajili wa kufuru katika kuelekea msimu ujao kama ilivyokuwa kwa Yanga chini ya wadhamini wake Kampuni ya GSM.
Habari zinaeleza Simba imepanga kufanya usajili wake kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji ambazo ndiyo zimeonekana kuwa na upungufu mkubwa.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa safu ya kiungo hawaifikirii kwa hivi sasa na hiyo ni kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kati ya hao wapo wanaomaliza mikataba yao ambao wamepanga kuwaongezea.
“Tuna idadi kubwa ya viungo wachezeshaji na washambuliaji katika timu yetu, labda kama tukiongeza ni kiungo mkabaji pekee yenye wachezaji wawili ambao ni Jonas Mkude na Mzamiru Yassin.
“Nguvu kubwa tumeelekeza katika kuiboresha safu ya ulinzi na ushambuliaji pekee, kwani ndiyo ambazo kocha ameziona zina upungufu katika msimu huu.
“Ngumu kusajili viungo wakati wapo wengi katika timu na tayari Sheva amepona na ameanza mazoezi magumu na mepesi ufukweni kwa ajili ya kujiweka fiti. Tunatarajia kumuona baada ya ligi kuanza,” amesema mtoa taarifa huyo.
Sheva alithibitisha hilo kwa kusema kuwa: “Nipo fiti hivi sasa kurejea uwanjani na subirieni kumuona Sheva mpya akirejea.
Chanzo:SpotiXtra