Home Uncategorized HIKI NDICHO AMBACHO KINAPANGWA KWA SASA KABLA YA LIGI KUREJEA

HIKI NDICHO AMBACHO KINAPANGWA KWA SASA KABLA YA LIGI KUREJEA


IKIWA imebaki wiki moja kufikia Juni Mosi, mwaka huu siku ambayo ligi za hapa nchini zitarejea, Serikali, Bodi ya Ligi (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jumamosi walikutana na kujadili namna gani wataweza kudhibiti Virusi vya Corona pindi michezo hiyo itakapoanza.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo alikuwepo kwenye kikao hicho maalumu kwa ajili ya kuona namna gani wataweza kupambana na Virusi vya Corona viwanjani na kutaka kujua Wizara ya Afya wamejipangaje na jambo hilo kabla ya kuanza kwa ligi zenyewe.
Kikao hicho ambacho kilizikutanisha Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Afya pamoja na viongozi wa TFF na wa Bodi ya Ligi, kilifanyika katika Ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) zilizopo Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Singo alisema, hakikuwa kikao cha kutoa ratiba ya ligi, bali walitaka kujua ni vitu gani ambavyo vitahitajika kwa wanamichezo na mashabiki katika wakati huu wa kupambana na Virusi vya Corona, licha ya kuwa TFF na TPLB walikaribishwa kusikiliza mchakato huo ili na wao wajue wanaisaidia vipi Serikali wakati michezo hiyo itakapoanza.
“Kikao chetu hakikuwa cha kupanga ratiba kwa sababu wanaohusika na hizo ratiba na muundo wa ligi ni TFF na TPLB na mamlaka za soka zinazohusika, sisi kikao chetu ilikuwa ni kujadili misingi ya kiafya itakuwaje pindi ligi itakapoanza.
“Yaani tunajadili ni mfumo gani ambao utakuwa sahihi kuutumia ambao utakuwa unazilinda klabu, wachezaji na mashabiki wakati wa ligi, kwa hiyo TFF na BMT wao tumekaribisha kuja kusikiliza kile ambacho sisi tunakijadili, mambo ya ratiba na ligi itakuwaje hiyo ipo juu ya TFF na Bodi ya ligi wenyewe,” alisema Singo.
Ikumbukwe kuwa, baada ya kutangazwa michezo kuendelea Juni Mosi, mwaka huu, imepangwa Ligi Kuu Bara kuchezwa Uwanja wa Taifa, Uhuru na Azam Complex jijini Dar, huku Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kuchezwa Nyamagana na CCM Kirumba jijini Mwanza.
SOMA NA HII  ORODHA YA NYOTA SABA WA SIMBA WATAKAOIKOSA DABI LEO KWA MKAPA