Mechi za kirafiki zimeweza kuonyesha picha ya kile ambacho wachezaji walikuwa wakikikosa kwa muda mrefu hata hamasa ya mashabiki nayo imeonekana ni kubwa.
Tangu Machi 17 hakukuwa na mechi yoyote ya ushindani na sababu kubwa ilikuwa ni janga la Virusi vya Corona ambavyo vinaivurugavuruga dunia.
Kwa kuamua kupambana na janga hilo Serikali iliamua kusimamisha masuala ya michezo ili kuepusha mikusanyiko isiyo ya lazima.
Baada ya mapambano ya muda mrefu, hatimaye Serikali imeridhia masuala ya michezo kuendelea na iliruhusu masuala hayo kuanza Juni Mosi huku ikisisitiza lazima tahadhari zichukuliwe.
Kwa kuwa wachezaji walikaa nje ya uwanja muda mrefu, benchi la ufundi limeamua kutumia mechi za kirafiki kutambua makosa yalipo ili watakapoanza mechi za ushindani wafanye vizuri.
Lakini tunaamini kuwa maandalizi ambayo timu zimefanya hakika tutashuhudia soka safi na lenye ubora na kupitia michezo hii ya kirafiki makocha wataangalia ni wapi zaidi wanatakiwa kupafanyia kazi zaidi ilikuleta ushindani na kupata matokeo.
Pia urejeo wa ligi hii itatoa picha halisi kwa wachezaji kama kweli walijituma kwa kuwa fiti au walikuwa wamebweteka wakati wa mapumziko ya lazima yaliyotokana na janga la Corona.