Michezo Bongo

‘Play Off’ Polisi TZ Katika Njia Za Ihefu Na Mashujaa? Prisons Ni Heshima Tu

Vardo July 11, 2026 11:20 am

WAKATI wadau na mashabiki wa soka nchini wakisubiri matokeo ya kuamua timu ya kucheza Ligi Kuu ya NBC msimu ujao kupitia mchujo wa mwisho, Polisi Tanzania inasaka rekodi ya Ihefu na Mashujaa, huku Tanzania Prisons ikipigania heshima yake.

Hii ni kutokana na timu hizo kutarajia kukutana katika mchezo wa mtoano wa mwisho baada ya hatua ya kwanza kumalizika kwa Mbeya City kubaki Ligi Kuu na Mbeya Kwanza kubaki Championship.

Katika hatua ya mtoano ‘Play Off’ wa kwanza upande wa Championship, Polisi Tanzania iliichakaza Mbeya Kwanza jumla ya mabao 7-1 na kufuzu hatua inayofuata, huku upande wa ligi kuu, Mbeya City ikiilima Prisons mabao 2-0.

Prisons iliyoshiriki Ligi Kuu msimu uliomalizika Juni 30, 2026, ilimaliza nafasi ya 13 kwa pointi 32, huku Mbeya City ikikamata nafasi ya 14 kwa pointi 32.

Kwa upande wa Polisi Tanzania ilimaliza Championship nafasi ya tatu kwa pointi 66 huku Mbeya Kwanza ikimaliza nafasi ya nne kwa pointi 61.

Polisi Tanzania inatarajia kuanzia nyumbani mchezo wa kwanza wa mtoano utakaopigwa uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro ikiikaribisha Prisons, Jumapili hii Julai 12, kisha kurudiana uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Julai 16 kujua hatma ya nani ataungana na timu zingine 15 kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026-2027.
SHUGHULI IKO HAPA

Polisi Tanzania imefikisha misimu mitatu haijacheza Ligi Kuu tangu iliposhuka daraja msimu wa 2022-2023 ambapo kwa sasa ina matarajio na matumaini ya kukata kiu ya mashabiki wake.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Polisi Tanzania, imekuwa na matokeo mazuri kwenye Championship hali inayowapa hamasa ya kufikia malengo yao na kukata kiu yao.

Katika mechi 30 ilizocheza za Championship, imefunga mabao 50 na kuruhusu 21 ambapo kwa wastani ni kama imefunga bao kwa kila mechi na kuwapa nguvu kufanya kitu kwa Prisons.

Hata hivyo, licha ya morali iliyopo kwa Polisi Tanzania, Tanzania Prisons nao si wanyonge kutokana na rekodi ya michezo sita ya mwisho wakifanikiwa kushinda tano na kupoteza moja.

Katika michezo hiyo, timu hiyo imekuwa na uhakika wa kufunga bao hali inayowafanya kujiamini zaidi kwamba wanaweza kupata mtaji wa bao kwenye mechi hiyo ya kwanza ugenini.
REKODI NA HESHIMA

Tanzania Prisons inawakabili Maafande wenzao ikiwa na kumbukumbu ya kucheza play off na timu ya Championship ikifanya hivyo msimu wa 2021-2022 ilipopepetana dhidi ya JKT Tanzania.

Katika mchezo wa kwanza, Prisons ikiwa ugenini uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ilishinda bao 1-0 na marudio kwenye uwanja wa Sokoine kulazimishwa sare ya bao 1-1 na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1.

Kutokana na historia hiyo, Wajelajela hao watakuwa wakisaka heshima si tu kubaki Ligi Kuu bali hata kuwaheshimisha mashabiki na wadau wake kuonesha ukongwe na uwezo kwenye soka dhidi ya wapinzani.

Utamu zaidi utakuwa kwa Polisi Tanzania inayosaka rekodi kuungana na timu za Ihefu na Mashujaa zilizofanya kweli kwa kupanda daraja kwa kuzifunga timu za Ligi Kuu na kuweka historia ya kipekee.

Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars) ilifanya hivyo msimu wa 2021-2022 ilipoitungua Mbao FC ya jijini Mwanza baada ya sare ya jumla ya mabao 4-4 huku ikinufaika na mabao mawili ya ugenini, ambapo mechi ya kwanza ilishinda 2-0 kisha kufungwa 4-2.

Mashujaa ya mkoani Kigoma ikiwa Championship iliinyuka Mbeya City mabao 4-1 baada ya mchezo kwanza kushinda 3-1 kisha wa marudiano kutakata bao 1-0 na kuandika historia.

VITA YA MAKATA NA NSAJIGWA

Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata ndiye kinara wa kupandisha timu Ligi Kuu akifanya hivyo kwa timu nne, ambapo awali alianza na Alliance FC ya jijini Mwanza (2017-2018), Polisi Tanzania (2018-2019), Dodoma Jiji (2019-2020) na Pamba Jiji (2023-2024).

Kwa sasa ndiye anaiongoza timu hiyo kwa mara ya pili akisaka rekodi na heshima nyingine katika medani za soka akiamini uwezo na uzoefu wake unaweza kumsaidia kufikia malengo hayo.

Shadrack Nsajigwa ndiye Kocha wa Tanzania Prisons, huu ndio msimu wake wa kwanza kuongoza timu ya Ligi Kuu akiwa kocha mkuu licha ya kwamba alishakaa benchi kwa timu za daraja hilo ikiwa ni Namungo alipokuwa kocha msaidizi.

Nsajigwa aliyecheza soka kwa mafanikio timu za Yanga na Taifa Stars, alitua Tanzania Prisons akitoka Transit Camp ya Championship na sasa anasaka rekodi na heshima ya kwanza kwenye mpira.

SIKIA KAULI ZAO

Makata anasema wanaiheshimu sana Prisons lakini wamejipanga kufanya vizuri haswa mchezo wa kwanza nyumbani wakihitaji idadi kubwa ya mabao ili kuwapa nguvu kwenye mchezo wa marudio.

Amesema amewaandaa vyema nyota wake kuhakikisha mechi hiyo hawachezi kujilinda isipokuwa ni kushambulia mwanzo mwisho ili kufikia malengo akibainisha kuwa shujaa hapatikani nyakati rahisi bali zile ngumu.

“Tunawaheshimu ila tutapambana nao kwa uwezo wetu, tunajua ni mchezo wa mtoano hivyo hatuna sababu ya kucheza kwa kujilinda bali kushambulia kutafuta idadi kubwa ya mabao ili ituweke salama.

“Vijana wako fiti na ukizingatia tumekuwa na matokeo mazuri tangu mzunguko wa pili wa Championship tukishinda mechi 14 katika ya 15, hali ambayo imetupa kujiamini kuisaka heshima upya na kukata kiu,” amesema Makata.

Makata ameongeza kuwa siri ya mafanikio ni umoja na ushirikiano baina ya wachezaji, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki ambao kila mmoja amefanya kwa nafasi yake akisisitiza kuwa wanaitaka Ligi Kuu.

Kwa upande wa Nsajigwa, amesema baada ya kukwepa kushuka daraja moja kwa moja, hatua waliyofikia ni fursa kubwa kwao kujitetea kwa nguvu zote kuhakikisha wanabaki salama Ligi Kuu.

Amesema licha ya matokeo waliyopata kutokuwa mazuri lakini ari na morali kikosini inawapa hamasa wachezaji na benchi la ufundi kupambana dakika zilizobaki kupigania nembo ya timu.

“Bado tunayo nafasi kwakuwa hatukuwa na mwanzo mzuri, niwapongeze wachezaji kwa namna walivyopambana hadi kubaki salama kwa sasa tukiamini bado tunaweza kufikia malengo,” amesema Nsajigwa.

Nahodha wa Tanzania Prisons, Lambart Sabiyanka amesema licha ya kuondoshwa kwenye play off ya kwanza, lakini si kwamba wamepoteza nafasi bali dakika 180 zilizobaki zinaweza kuwaheshimisha tena.

“Kimsingi tuna ushirikiano nab ado hatjakata tamaa, tunaamini kwa mechi zilizobaki tunaenda kupambana kadri tuwezavyo kuinusuru timu kushuka daraja, haijaisha hadi iishe,” amesema kiungo huyo.

Mbili Za Ligi Kuu Zamuwania Ladaki Chasambi Kukosa Penalti Janga Kombe La Dunia