Kalesto Afungua Njia Ya Loemba Kuondoka Simba.
UONGOZI wa Simba unatajwa kuendelea kufanya maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27, huku kiungo Inno Loemba akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuondoka ndani ya kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko yanayofanywa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Steve Barker, linalolenga kuimarisha kikosi kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.
Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na klabu hiyo, Simba inapanga kuachana na Loemba ili kufungua nafasi ya usajili wa mchezaji wa kimataifa, huku winga wa Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, akidaiwa kuwa amekamilisha taratibu za kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
“Kuondoka kwa Loemba kutafungua nafasi ya mchezaji mpya wa kimataifa. Simba inaendelea kukiboresha kikosi chake kwa lengo la kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Hadi sasa uongozi wa Simba haujatoa tamko rasmi kuhusu hatma ya Loemba wala kukamilika kwa usajili wa Makgalwa, hivyo mashabiki wanaendelea kusubiri uthibitisho rasmi kutoka klabuni.